ZARA ADVENTURES TOURS TANZANIA YAONESHA UBORA WA HUDUMA ZAKE KATIKA MAONYESHO YA KILIFAIR 2026 ARUSHA.

Geofrey Steven
3 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

KAMPUNI ya Zara Adventures Tours Tanzania imeendelea kung’ara katika Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii ya KiliFair 2026 yanayofanyika jijini Arusha, huku ikionyesha uwezo wake mkubwa wa kuwahudumia wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania waliofika kushiriki maonyesho hayo.

Akizungumza katika viwanja vya Magereza, Arusha, ambako maonyesho hayo yanafanyika, Nacy Mbotea ambaye ni miongoni mwa watumishi wa Zara Adventures Tours Tanzania, alisema kampuni hiyo imefurahishwa na mafanikio ya KiliFair 2026 pamoja na mchango wake katika kukuza sekta ya utalii nchini.

Habari Picha 18632
Habari Picha 18630

Nacy alisema kuwa Zara Adventures Tours Tanzania, kama mmoja wa wadau na washiriki wa maonyesho hayo, imeridhishwa na maandalizi na uendeshaji wa KiliFair 2026 ambao umewezesha kuwakutanisha wadau wa utalii kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.

“Tumefurahi kuona wageni na washiriki kutoka mataifa mbalimbali wakifika nchini Tanzania kushiriki maonyesho haya.

Hii inaonesha jinsi Tanzania inavyoendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii duniani na jinsi sekta hii inavyozidi kukua kila mwaka,” alisema Nacy.

Habari Picha 18633

Aliongeza kuwa Zara Adventures Tours Tanzania ni miongoni mwa wadhamini wa Kilimanjaro Summit Challenge, programu maalum inayowapa washiriki wa KiliFair fursa ya kushiriki safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Nacy, ushiriki wa kampuni hiyo katika Kilimanjaro Summit Challenge umechangia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia utalii wa mlima, michezo ya nje na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya utalii duniani.

Habari Picha 18634

Aidha, alitoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa zinazoendelea kufanyika katika kuimarisha na kutangaza utalii wa Tanzania katika soko la kimataifa.

“Tunaendelea kushuhudia matokeo chanya ya juhudi hizi. Idadi ya watalii wanaofika nchini inaongezeka, na matukio makubwa kama KiliFair yanafungua fursa zaidi za biashara, uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya utalii,” alisisitiza.

Habari Picha 18635

Nacy pia aliwashukuru waandaaji wa KiliFair 2026, washirika, wadhamini na wadau wote waliofanikisha maonyesho hayo pamoja na Kilimanjaro Summit Challenge, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia kuimarisha taswira ya Tanzania kama moja ya nchi bora za utalii duniani.

Alisema Zara Adventures Tours Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza utalii endelevu na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha vivutio vya utalii barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment