CRDB YAENDELEA KUIMARISHA AFYA, MICHEZO NA USHIRIKIANO WA JAMII KUPITIA POLISI JAMII JOGGING CLUB

Geofrey Steven
4 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

Benki ya CRDB Plc imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuunga mkono shughuli za kijamii, afya na maendeleo ya wananchi kwa kukabidhi msaada wa tisheti 500 pamoja na mipira minne ya michezo kwa Polisi Jamii Jogging Club ya Arusha.

Msaada huo ulikabidhiwa rasmi na Meneja wa Kanda wa CRDB, Cosmas Sadat, kwa mlezi wa klabu hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Georgina Matagi,

Habari Picha 18528

katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Polisi Wilaya ya Arusha. Hafla hiyo ilihudhuriwa na askari polisi pamoja na wananchi mbalimbali waliojitokeza kushuhudia tukio hilo muhimu.

Habari Picha 18530

CRDB Yaona Michezo ni Chachu ya Afya na Mshikamano.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Cosmas Sadat alisema kuwa CRDB inaamini michezo na mazoezi ni nyenzo muhimu katika kuimarisha afya za wananchi, mshikamano wa jamii pamoja na kujenga mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.

Alieleza kuwa benki hiyo imekuwa mshirika wa karibu wa Polisi Jamii Jogging Club kupitia utoaji wa elimu ya fedha, huduma za biashara na uwezeshaji wa vikundi mbalimbali vya kijamii ili kusaidia wananchi kuinuka kiuchumi.

 

Habari Picha 18531

“CRDB itaendelea kushirikiana na jamii kupitia shughuli mbalimbali zinazolenga afya, maendeleo na ustawi wa wananchi,” alisema Sadat.
Arusha Jogging Club Yatajwa Kuwa Mfano wa Mafanikio.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha, ACP Salvas Makweli, alisema Polisi Jamii Jogging Club ya Arusha imeendelea kuwa mfano wa mafanikio nchini kutokana na ukuaji wake mkubwa, ushiriki mpana wa wananchi pamoja na uwezo wake wa kuvutia wadhamini mbalimbali.

ACP Makweli alisema klabu hiyo imejizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya Mkoa wa Arusha kupitia shughuli zake zinazorushwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Habari Picha 18532
Habari Picha 18533

“Kwa sasa club iko live sana. Ukiangalia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii utaona namna Arusha Jogging Club ilivyopata nguvu kubwa,” alisema ACP Makweli.

Aidha, alimpongeza Georgina Matagi pamoja na viongozi wa klabu hiyo kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya katika kuimarisha shughuli za kijamii kupitia michezo, huku akiishukuru CRDB kwa kuendelea kuwa mdhamini muhimu wa klabu hiyo.

Michezo Yatajwa Kuunganisha Jamii.

ACP Makweli aliongeza kuwa michezo imeendelea kuwa daraja muhimu la kuunganisha jamii, kuimarisha afya za wananchi na kutoa fursa kwa vijana kukuza vipaji vyao.

Alisema Polisi Jamii itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha michezo inakuwa sehemu ya kuchochea maendeleo, mshikamano na usalama wa jamii.

Georgina Matagi Aipongeza CRDB.

Naye mlezi wa Polisi Jamii Jogging Club ambaye pia ni OCD wa Arusha, Georgina Matagi, alisema klabu hiyo imekuwa kiungo muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi kupitia michezo na mazoezi ya pamoja.

Matagi alisema klabu hiyo yenye wanachama zaidi ya 300 imekuwa ikifanya mazoezi kila Jumamosi asubuhi huku ikihamasisha afya bora, amani, mshikamano pamoja na mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu katika jamii.

Habari Picha 18534
Habari Picha 18535

Aliishukuru CRDB kwa kuendelea kuwa mdhamini mkubwa wa klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia mafanikio makubwa ya Polisi Jamii Jogging Club Arusha.

“Msaada huu utasaidia kuongeza hamasa kwa wanachama wetu na kuendeleza shughuli mbalimbali za kijamii tunazozifanya kupitia klabu hii,” alisema Matagi.

Wanachama Wafurahishwa na Msaada.

Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo walieleza kufurahishwa na msaada huo wakisema utawapa motisha zaidi ya kushiriki mazoezi pamoja na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa kupitia klabu hiyo.

Habari Picha 18537

 

Habari Picha 18536

Polisi Jamii Jogging Club ya Arusha imeendelea kuvutia mamia ya wananchi kushiriki mazoezi ya pamoja kila wiki, huku ikijijengea sifa ya kuwa moja ya klabu zinazochochea afya bora, umoja na maendeleo ya kijamii katika Mkoa wa Arusha.

Mwisho….

Share This Article
Leave a Comment