JAI Yagusa Mioyo ya Wagonjwa kwa Chakula na Dua Hospitali ya Wilaya ya Hai wakati wa Eid Al Adha

Geofrey Steven
2 Min Read

Hai, Kilimanjaro

Jumuiya ya Jamiiyatul Akhlaaqul Islaamu (JAI) ya Bomang’ombe, Msikiti wa Matopeni Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, imetembelea Hospitali ya Wilaya ya Hai na kufanya matendo ya huruma kwa wagonjwa kwa kutoa chakula pamoja na zawadi mbalimbali katika kipindi cha maadhimisho ya Eid Al Adha.

Akizungumza baada ya zoezi hilo lililofanyika Mei 28, 2026, Mwamasishaji wa JAI, Kileo Omar, amesema kuwa jumuiya hiyo imekuwa na utaratibu wa kuwafikia wagonjwa hususan nyakati za sikukuu ili kuwafariji na kuungana nao.

Habari Picha 18517
Habari Picha 18516

“Ku watembelea wagonjwa ni jambo jema sana. Tunapoungana nao katika kipindi hiki cha sikukuu, wanapata faraja na kujiona kuwa sehemu ya jamii. Hata vitabu vitakatifu vinatuhimiza kufanya hivyo,” amesema Kileo.

Amesema kuwa tendo hilo ni la kiimani na linaashiria upendo, mshikamano na umoja katika jamii. Aidha, alieleza kuwa JAI imekuwa mstari wa mbele kusaidia watu wenye uhitaji, wakiwemo wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za dawa.

“Tumekuwa tukisaidia baadhi ya wagonjwa kununua dawa pale wanaposhindwa kutokana na ukosefu wa fedha. Hii ni sehemu ya wajibu wetu kwa jamii,” ameongeza.

Habari Picha 18518

Kwa upande wake, Fortunatus Kisheo, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, ameipongeza JAI kwa moyo wa kujitolea na kuamua kusherehekea Eid Al Adha pamoja na wagonjwa hospitalini hapo.

“Tunawapongeza sana kwa jambo hili mlilolifanya. Tunafahamu kuwa mngeweza kwenda sehemu nyingine nyingi, lakini mmeamua kuja hapa hospitalini kuwafariji wagonjwa na kushiriki nasi huduma hii muhimu,” amesema Kisheo.

Ameongeza kuwa msaada huo umeleta faraja kubwa kwa wagonjwa pamoja na watumishi wa hospitali hiyo.

“Nyinyi mnatoa huduma za kiroho na sisi tunatoa huduma za kimwili. Mwenyezi Mungu awabariki kwa moyo wenu wa upendo na mshikamano. Tunawaomba muendelee kufika hata siku nyingine,” amesisitiza.

Wagonjwa pamoja na baadhi ya ndugu waliokuwepo hospitalini hapo walionyesha furaha yao kwa kupatiwa chakula na kushirikishwa katika maombi maalum yaliyofanywa na viongozi wa JAI.

Habari Picha 18519

Matendo hayo ya huruma yanaendelea kuwa mfano mzuri wa mshikamano wa kijamii na kusaidia kuleta matumaini kwa watu wenye uhitaji katika jamii.

Mwisho

Share This Article
Leave a Comment