Na Geofrey Stephen Arusha .
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC limempongeza Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Mheshimiwa Dkt. Joanes Lukumay, kwa kutoa fedha za Mfuko wa Jimbo kiasi cha shilingi milioni 79.761 kwa kata 11 za jimbo hilo kwa lengo la kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na maendeleo.
Fedha hizo zimeelekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya,

elimu, miundombinu ya barabara pamoja na huduma nyingine muhimu zinazogusa maisha ya wananchi wa Arumeru Magharibi.
Wakizungumza katika kikao cha baraza hilo, madiwani walieleza kuwa hatua ya Mbunge Lukumay kutoa fedha hizo inaonesha dhamira yake ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Kwa upande wake, Mbunge Dkt. Joanes Lukumay alisema fedha hizo zimepelekwa moja kwa moja katika kata husika ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa haraka bila kusubiri utekelezaji wa bajeti kuu ya Serikali.
Alieleza kuwa baadhi ya changamoto zinazohitaji hatua za haraka ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, huduma za afya, mazingira ya elimu pamoja na mahitaji mengine ya msingi kwa wananchi.

Aidha, viongozi mbalimbali katika halmashauri hiyo walimpongeza Mbunge huyo kwa kuendelea kushirikiana na madiwani pamoja na wananchi katika kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya Arumeru Magharibi.


Baraza hilo pia liliwataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo pamoja na kulinda miradi inayotekelezwa kwa manufaa ya jamii nzima.
Mwisho……
