Na Mwandishi wa A24tv.
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Hassan Bomboko, ametembelea maeneo yaliyoathirika na mvua kubwa ikiwemo Kata ya Kia (kijiji cha Tindigani), Mtakuja, Sanya Station, Gezaulole pamoja na baadhi ya maeneo ya Kata ya Muungano.
Akizungumza Machi 28, 2026 baada ya ziara hiyo, Bomboko alieleza kuwa moja ya sababu kubwa ya athari za mafuriko ni ujenzi holela unaokiuka taratibu za mipango miji. Alibainisha kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakijenga kwenye njia asilia za maji kama mito midogo na mabonde, hali inayozuia maji kupita kwa urahisi na hivyo kusababisha mafuriko yanayoathiri makazi na miundombinu.


“Tumegundua kuwa katika maeneo mengi ya mijini, wananchi hawazingatii mipango miji na kujenga katika maeneo ambayo awali yalikuwa njia za maji. Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa athari za mafuriko,” alisisitiza Bomboko.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amezielekeza mamlaka za miji midogo pamoja na viongozi wa kata, wakiwemo madiwani na wenyeviti wa vitongoji, kushirikiana na wananchi kuhakikisha maeneo yaliyozibwa yanafunguliwa upya ili kuruhusu upitishaji wa maji kupitia mitaro.
Aidha, ameiagiza TARURA kufanya tathmini ya haraka ya miundombinu iliyoathirika, pamoja na kuchukua hatua za kuchimba mitaro na kukarabati barabara ili kurejesha hali ya kawaida na kuzuia madhara zaidi.
Bomboko aliahidi kuwa ofisi ya wilaya itashughulikia changamoto zote zilizotokana na mvua hizo, ikiwemo uharibifu wa barabara, mifereji na makazi, huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kurejesha huduma muhimu kwa haraka na ufanisi.


Pia aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, kufuata maelekezo ya wataalamu, na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapoona viashiria vya hatari ili hatua stahiki zichukuliwe mapema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bomang’ombe, Evod Njau, alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutembelea maeneo hayo na kuahidi kushirikiana na wananchi katika kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa mitaro, hatua itakayosaidia kupunguza athari za mafuriko wakati wa mvua.
Mwisho

