Na Mwandishi wa A24tv .

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, , maarufu kwa jina la “Bwege,” amefariki dunia mchana wa leo, Machi 30, 2026, katika hospitali binafsi iliyopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Taarifa za msiba huo zimethibitishwa na kaka wa marehemu, Abbas S.A. Bungara, ambaye amesema kuwa ndugu yake alifariki akiwa hospitalini hapo akipatiwa huduma ya kusafisha damu (dialysis), huduma ambayo alikuwa akiipata mara kwa mara kutokana na hali yake ya kiafya.
Akizungumza na vyombo vya habari, Abbas ameeleza kuwa matibabu yalikuwa yakiendelea kama kawaida kabla ya hali ya marehemu kubadilika ghafla na hatimaye kupoteza maisha.
Kwa sasa, familia inaendelea na maandalizi ya mazishi, huku taarifa zaidi kuhusu ratiba na taratibu za mazishi zikitarajiwa kutolewa baadaye. Msiba umewekwa nyumbani kwa Abbas Bungara, eneo la Temeke, Dar es Salaam, ambako ndugu, jamaa na marafiki wanaendelea kufika kutoa pole.
Enzi za uhai wake, Bungara alijulikana sana katika siasa za Tanzania kwa msimamo wake thabiti pamoja na mtindo wake wa kipekee wa kuchanganya hoja nzito na ucheshi alipokuwa akichangia mijadala bungeni.
Katika safari yake ya kisiasa, aliwahi kuwa mwanachama wa vyama mbalimbali ikiwemo CUF na ACT-Wazalendo. Hivi karibuni, alitangaza kuhamia CHADEMA, ingawa mchakato wa kukabidhiwa rasmi kadi ya chama hicho ulikuwa bado haujakamilika.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia, wafuasi wake wa kisiasa na jamii kwa ujumla.
Mwisho…

