PICNIC LOUNGE YAUNGANA NA JAMII KUENZI KUMBUKUMBU YA DANIEL JOSEPH KWA MISA TAKATIFU NA UPANDAJI MITI ARUSHA.

a24tv
3 Min Read

Na  GEOFREY STEPHEN ARUSHA

Siku chache baada ya kifo cha kijana Daniel Joseph aliyefariki kufuatia kubebwa na maji katika Kata ya Muriet (Terrat), familia yake kwakushirikiana na ndugu, jamaa na marafiki wamefanya misa takatifu ya shukrani sambamba na zoezi la upandaji miti kama sehemu ya kuenzi maisha yake.

Habari Picha 11611
Habari Picha 11610

Tukio hilo lilifanyika tarehe 22 Machi 2026 katika kigango cha Mt. Mathias Lumba kilichopo Terrat, Jijini Arusha. Misa hiyo iliongozwa na Padri Eustachius Kajungi, ambaye katika mahubiri yake alisisitiza kuwa marehemu Daniel Joseph alikuwa kiongozi mwenye bidii katika shughuli za kanisa akiwa kijana.

Padri Kajungi alieleza kuwa upandaji wa miti ya matunda ni ishara ya kudumu ya mchango wa Daniel katika kanisa na jamii, akibainisha kuwa alama hiyo itaendelea kuwakumbusha vizazi vya sasa na vijavyo juu ya huduma na moyo wake wa kujitolea.

Habari Picha 11612
Habari Picha 11613

Kwa upande wake, baba mzazi wa marehemu, Joseph Massawe (maarufu kama Kona), alisema kuwa lengo la kupanda miti hiyo ni kuweka kumbukumbu ya kudumu ya mtoto wao aliyefariki tarehe 27 Februari 2026, na kuzikwa Rombo tarehe 4 Machi 2026.

“Tutamkumbuka sana mtoto wetu. Alikuwa mtumishi wa kanisa mwenye ndoto kubwa ya kusaidia na kuimarisha huduma.

Kila tutakapoiona miti hii, tutakumbuka moyo wake wa kujitolea,” alisema kwa huzuni.

Zaidi ya miche 18 ya miti ya matunda ilipandwa katika eneo la kanisa hilo, huku waumini waliohudhuria wakieleza kufurahishwa na hatua ya familia kuunganisha ibada ya shukrani na tendo la kupanda miti kama kumbukizi ya kijana huyo.

Habari Picha 11614

Walieleza kuwa tukio hilo si tu limeonyesha upendo wa familia kwa marehemu, bali pia limeacha alama yenye manufaa kwa jamii, hasa ikizingatiwa kuwa miti hiyo itazaa matunda kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Picnic Lounge ya Jijini Arusha, Antony Urasa, pamoja na Stephen Lyimo maarufu kama “Mzee Lyimo”. Wote kwa pamoja walieleza kuwa waliguswa na maisha ya marehemu na mchango wake kanisani, hivyo waliona ni muhimu kushiriki tukio hilo la heshima

Habari Picha 11616
Habari Picha 11615

Kwa hakika, kumbukizi ya Daniel Joseph itaendelea kuishi si tu mioyoni mwa watu, bali pia kupitia miti hiyo ya matunda — ishara ya uhai, matumaini na urithi wa upendo aliouacha duniani.

Habari Picha 11618
Habari Picha 11617
Habari Picha 11619

Mwishoo

Share This Article
Leave a Comment