WAISLAMU WASISITIZWA KUENDELEZA MEMA BAADA YA RAMADHANI

a24tv
2 Min Read

Na Mwandishi A24tv .

Naibu Imamu wa Msikiti wa Shafiy, Boma Ng’ombe Wilayani Hai, Mahmoud Omar, amewasihi Waislamu pamoja na wananchi kwa ujumla kuendeleza matendo mema hata baada ya kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Habari Picha 11592

Akizungumza wakati wa hotuba ya Sikukuu ya Idd El-Fitr iliyofanyika Machi 21, 2026, kimkoa Wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, na kuhudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, Mahmoud alisisitiza umuhimu wa kudumisha mema yaliyofanywa kipindi cha Ramadhani.

Habari Picha 11587
Habari Picha 11588

Katika hotuba yake, aliwataka waumini kuepuka kurejea katika matendo maovu, akieleza kuwa ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

“Ni kweli licha ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kumalizika, Waislamu na wananchi kwa ujumla endelezeni matendo mema yaliyofanywa kipindi cha mwezi huo,” alisema Mahmoud.

Alifananisha mwezi wa Ramadhani na semina, akieleza kuwa mafunzo yaliyopatikana yanapaswa kuendelea kutumika katika maisha ya kila siku.
Mahmoud alisema amelazimika kutoa wito huo kufuatia taarifa kuwa baadhi ya watu hurudi katika matendo maovu mara tu baada ya kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani.

Aliongeza kuwa wakati wa Ramadhani, waumini walijitahidi kuswali, kusoma Qur’an na kutoa sadaka kwa wenye uhitaji, hivyo ni vyema kuendeleza matendo hayo ili kupata baraka za Mwenyezi Mungu.

Habari Picha 11589
Habari Picha 11590
Habari Picha 11591

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mlewa Shaabani, alisisitiza umuhimu wa kuwapatia watoto elimu ya dini, akibainisha kuwa elimu hiyo huwajenga kuwa watu wema katika jamii.
Aidha, aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani nchini.

**Mwisho

Share This Article
Leave a Comment