na Geofrey Stephen .ARUSHA:
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya ya msingi nchini, huku ikiendelea kuongeza uwekezaji katika miundombinu, wataalamu na rasilimali nyingine muhimu za afya.
Dkt. Nchemba amesema hayo Septemba 9, 2026 wakati akifungua kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Afya ya Msingi unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Amesema mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya, hususan katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, yameifanya Tanzania kutambulika kimataifa.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, mafanikio hayo yamechangia Rais Samia kutunukiwa Goalkeeper Award mwaka 2025, pamoja na kuteuliwa kuwa kinara wa Umoja wa Afrika katika huduma za afya ya mama na mtoto mwaka 2026.
Dkt. Nchemba amesema Serikali sasa inaelekeza nguvu zaidi katika kuboresha ubora na ufanisi wa huduma za afya, sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati.
Amesema vifo vitokanavyo na uzazi duniani vimepungua kutoka takribani 328 hadi 197 kwa kila vizazi hai 100,000 kati ya mwaka 2000 na 2023, akisisitiza kuwa malengo ya afya yanaweza kufikiwa kupitia uwekezaji mkubwa na utekelezaji wa mipango madhubuti.

ZAIDI YA WATUMISHI 16,000 WA AFYA WAJIRIWA
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuongeza wataalamu katika sekta ya afya, ambapo zaidi ya watumishi 16,000 wameajiriwa kati ya Desemba 2025 na mwaka 2026.
Aidha, amesema Serikali imejenga zaidi ya nyumba 430 za watumishi wa afya na inapanga kujenga takribani nyumba nyingine 2,000 kuelekea mwaka 2030.
Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha watumishi wa afya wanapata mazingira bora ya kazi na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi.
BIMA YA AFYA KWA WOTE
Dkt. Nchemba pia amesema utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote utasaidia wananchi, wakiwemo wenye kipato duni, kupata huduma bora za afya kwa gharama nafuu na bila ubaguzi wa kipato.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za afya bila kukabiliwa na changamoto kubwa za gharama.

VITUO 95.8% NI VYA AFYA YA MSINGI
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Silas Shemdoe, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba katika ngazi ya afya ya msingi.
Prof. Shemdoe amesema takwimu za mwaka 2025 zinaonesha umuhimu mkubwa wa vituo vya afya ya msingi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema kati ya wajawazito milioni 2.09 waliojifungulia katika vituo vya afya vya umma, milioni 2, sawa na asilimia 95.6, walipata huduma katika ngazi ya afya ya msingi.

Aidha, kati ya mahudhurio milioni 32.3 ya wagonjwa wa nje katika vituo vya afya vya umma, milioni 27.8, sawa na asilimia 86, yalifanyika katika vituo vya afya ya msingi.
Tanzania ina jumla ya vituo 8,288 vya afya vinavyomilikiwa na Serikali, ambapo 7,946, sawa na asilimia 95.8, ni vya ngazi ya afya ya msingi vinavyomilikiwa na Halmashauri.
TEHAMA YAONGEZA UFANISI
Prof. Shemdoe amesema Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika vituo vya afya.
Amesema asilimia 96.6 ya vituo vya afya ya msingi vimeunganishwa na mfumo wa GoTHOMIS, huku asilimia 87.6 vikiwa vimeunganishwa na mfumo wa GePG.
Amesema mifumo hiyo inasaidia kuongeza ufanisi, uwazi na usimamizi wa mapato pamoja na huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Aidha, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa dawa na bidhaa za afya ili kuhakikisha upatikanaji wake unaimarika katika vituo vya kutolea huduma.
Prof. Shemdoe amesema pia Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na uwajibikaji kupitia Mikoa, Wilaya na Halmashauri ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa unaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

ARUSHA YANUFAIKA NA UWEKEZAJI WA SH. BILIONI 94.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuutendea haki Mkoa wa Arusha katika eneo la afya ya msingi.
Mhe. Makalla amesema zaidi ya Sh. bilioni 94 zimeelekezwa katika kuboresha huduma za afya ya msingi mkoani humo, ikiwa ni pamoja na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya.
Amesema uwekezaji huo umechangia kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 382 hadi 450, huku Mkoa ukipokea magari 27 ya wagonjwa.
Aidha, amesema watumishi wapya 823 wa kada za afya wameajiriwa, hatua ambayo imechangia kuboresha huduma na kusaidia kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto.

Mhe. Makalla amewataka wananchi wa Arusha kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zinazotokana na ujio wa mikutano ya kitaifa na kimataifa mkoani humo.
Amesema Arusha ina miundombinu ya kutosha kuwezesha mikutano mikubwa na kuwataka Wizara, Taasisi na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa kuendelea kuchagua Arusha kuwa mwenyeji wa mikutano yao.
“Arusha tuna utalii wa mbugani na hapa ndipo kitovu cha kwenda Ngorongoro, Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Tarangire na maeneo mengine. Utalii mwingine ni utalii wa mikutano. Arusha ndiyo kitovu cha utalii wa mikutano ya kitaifa na kimataifa,” amesema Mhe. Makalla.
Aidha, amesema Mkoa wa Arusha uko tayari kunufaika na fursa za utalii wa michezo zinazotarajiwa kuongezeka kupitia Michuano ya AFCON 2027.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amesema Serikali imeendelea kuimarisha utalii wa matibabu, jambo linaloifanya Arusha kuwa eneo muhimu la huduma za afya kwa Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema yeye ni shahidi wa kazi kubwa inayotekelezwa na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya na miundombinu mkoani Arusha.
MKUTANO WA KIMATAIFA WA AFYA YA MSINGI.
Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Afya ya Msingi unaofanyika Arusha kuanzia Septemba 9 hadi 11, 2026, umewakutanisha wataalamu na wadau mbalimbali wa afya kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Mkutano huo unajadili namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi, ugharamiaji endelevu, ufanisi, ubora wa huduma na kujenga mifumo imara ya afya kwa lengo la kufikia Afya kwa Wote.
Mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu:
“Kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote: Kuimarisha ugharamiaji endelevu wa huduma za afya, ufanisi na uboreshaji wa huduma katika ngazi ya msingi.”

Mwisho……
