TEMESA YAKETI NA WADAU WA NISHATI YA UMEME.

Geofrey Steven
3 Min Read

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) leo tarehe 31,Agositi 2026 umeendesha kikao cha wadau cha kujadili fursa za matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme (FIRST E-MOBILITY MULTI-SECTORAL), kikao hicho kilicholenga kujadili maendeleo, fursa na changamoto katika matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme nchini Tanzania kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Makao Makuu TEMESA jijini Dodoma na kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka Serikali na sekta binafsi, wakiwemo watengenezaji, waagizaji na wasambazaji wa magari ya umeme pamoja na bajaji.

 

Akizungumza kwa Niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za ufundi, Mhandisi Julius Humbe amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kujenga mazingira wezeshi kwa maendeleo ya usafiri unaotumia nishati ya umeme nchini ili kupunguza matumizi ya nishati ya petroli na dizeli ambazo zimekuwa changamoto kubwa kwa sasa.

Habari Picha 20754

 

‘’Mtakumbuka kwamba kuna tatizo kubwa kuhusu bei za mafuta kupanda hivyo sisi kama wadau tumeona ni muhimu kuwakutanisha wadau ili tuweze kujadili kuhusu matumizi ya vyombo vyinavyotumia nishati ya umeme,kulingana na Dira yetu ya Maendeleo ya 2050, tunasema tunaenda kidigitali zaidi, tunatamani Serikali ipate magari yanayotumia umeme ili tuweze kupunguza gharama za uendeshaji katika Serikali yetu amesema Mhandisi Humbe”,

 

Humbe ameongeza kuwa teknolojia hiyo ya magari yanayotumia nishati ya umeme yanatumia kiasi kidogo sana cha nishati ya umeme na hivyo yatasaidia katika uendeshaji wa magari ya Serikali kwa kuwa kwa nishati kidogo tu ya umeme na magari hayo yanao uwezo wa kusafiri kwa zaidi ya kilometa 600 kwa mujibu wa wataalamu walioleta magari hayo kwa ajili ya kuyaonesha.

 

ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha teknolojia ya magari ya umeme inaendelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya nchi, usalama, viwango na upatikanaji wa miundombinu rafiki kwa watumiaji.

Habari Picha 20755

 

Aidha, wadau walijadili masuala mbalimbali yanayohusiana na miundombinu ya kuchajia magari ya umeme, matengenezo na huduma za kitaalamu, viwango na usalama wa magari ya umeme, upatikanaji wa vipuri pamoja na uendelezaji wa wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia ya E-Mobility.

Wadau hao waliishukuru TEMESA kwa kuwapatia fursa hiyo ya kuwakutanisha pamoja ili waweze kutangaza bidhaa zao za magari na vyombo vinavyotumia umeme.

Habari Picha 20753

 

Kikao hicho kimekuwa fursa kwa Serikali na wadau wa sekta binafsi kubadilishana uzoefu, kutambua changamoto zilizopo na kuweka msingi wa ushirikiano zaidi katika kukuza E-Mobility nchini Tanzania.

 

Miongoni mwa kampuni zilizoshiriki kikao hicho ni Dow Elef Auto Limited, BYD Tanzania (Harmony Auto Branch), JMC Tanzania (Transinnovation Motors Tanzania), Plug and Ride Company Limited, GAC Tanzania (HF Motors Tanzania), E Motion Africa Limited na Tanzania Jetour.

 

Habari Picha 20756

 

Mwisho…

Share This Article
Leave a Comment