Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Christopher Timbuka, amekutana na viongozi wa makundi mbalimbali katika jamii na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa chanjo ya polio itakayotolewa kwa watoto kwa njia ya matone.
Timbuka amesema jumla ya watoto kati ya 42,000 na 49,000 wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo katika Wilaya ya Siha, huku zoezi hilo likitarajiwa kuanza Agosti 27 hadi 30, 2026.
Akizungumza Agosti 24, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, wakati wa kutoa elimu kwa watu mashuhuri katika jamii, wakiwemo wazee wa kimila, waganga wa tiba asili, viongozi wa dini na viongozi wengine wa jamii, Timbuka alisema ushiriki wa makundi hayo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu zoezi hilo.

“Ni kweli mafunzo haya yanahusu zoezi la utoaji wa chanjo ya polio kwa njia ya matone, ambayo itatolewa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 10,” alisema Timbuka.
Alisema baadhi ya watendaji tayari wamepatiwa mafunzo kuhusu utekelezaji wa zoezi hilo, lakini viongozi wa jamii wamepewa elimu ili waweze kuwa mabalozi wa zoezi hilo katika maeneo yao.
“Hatukuona ni vyema zoezi hili liende katika maeneo yenu bila ninyi kufahamu kinachoendelea. Tunategemea kwamba mkipata taarifa sahihi, mtatusaidia kuelimisha jamii na kuhakikisha zoezi hili linaenda vizuri,” alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chanjo wa Wilaya ya Siha, Paul Izack, alisema zoezi la chanjo litaanza rasmi Agosti 27 na kumalizika Agosti 30, 2026, likifanyika katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu.
Izack alisema chanjo hiyo itatolewa bure katika maeneo mbalimbali, ikiwemo nyumba za ibada, shule za msingi na awali, masoko, maduka na maeneo mengine. Alisema hata watoto watakaokuwa mashambani pamoja na wazazi wao watapatiwa chanjo iwapo timu za chanjo zitawafikia huko.
Alieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuwalinda watoto dhidi ya virusi vya polio aina ya pili, vinavyoweza kusababisha ugonjwa wa kupooza ghafla kwa watoto.
“Ugonjwa wa polio ni hatari kwa sababu unasababishwa na virusi vinavyoweza kusababisha kupooza ghafla kwa viungo vya mwili, hususan mikono na miguu, na katika baadhi ya hali unaweza kusababisha kifo,” alisema Izack.
Alisisitiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto walio chini ya umri wa miaka 10 wanapatiwa chanjo hiyo pindi timu za chanjo zitakapowafikia katika maeneo yao.
Mwisho
