OLE MILYA AMPONGEZA MAVUNDE KUSIKILIZA KILIO CHA WADAU WA TANZANITE MIRERANI

Geofrey Steven
3 Min Read

SIMANJIRO, MANYARA

Mbunge wa Simanjiro na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa James Ole Milya, amempongeza Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, kwa kutenga muda wa kusikiliza changamoto na maoni ya wananchi pamoja na wadau wa sekta ya madini katika eneo la Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara.

Ole Milya amesema hatua ya Waziri Mavunde kufika Mirerani na kusikiliza kwa karibu changamoto zinazowakabili wananchi ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha rasilimali za nchi zinasimamiwa kwa manufaa ya Watanzania.

Habari Picha 20215

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Ole Milya amesema Tanzanite ni madini ya kipekee duniani ambayo yanapatikana Tanzania pekee, hivyo yanapaswa kupewa kipaumbele maalum katika kuhakikisha uchimbaji, biashara na mnyororo mzima wa thamani unawanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Kwa sababu linaitwa Tanzania, ni vyema tukaangazia macho yetu na kubeba bendera ya nchi kupitia madini haya,” amesema Ole Milya.

Amesema pamoja na Tanzanite kuwa na thamani kubwa kimataifa, shughuli za uchimbaji wake zinakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mahitaji ya mitaji, ugumu wa uchimbaji, masoko na biashara, hivyo Serikali inapaswa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji na wadau wengine wanaoshiriki katika sekta hiyo.

Ole Milya amesema wananchi wa Simanjiro wanataka kuona biashara ya Tanzanite ikikua kwa namna ambayo inanufaisha Taifa, wananchi na wadau wote wa mnyororo wa thamani, bila kuwaathiri wachimbaji ambao wamewekeza muda, nguvu na mitaji yao katika shughuli za uchimbaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kusikiliza sauti za wananchi mbalimbali wanaoshiriki katika shughuli za madini, wakiwemo wachimbaji wadogo, wanawake wanaojishughulisha na madini, wafanyabiashara na madalali.

Kwa mujibu wa Ole Milya, kusikiliza changamoto za makundi hayo ni muhimu katika kuhakikisha Serikali inapata picha halisi ya hali ya sekta hiyo na kuchukua hatua zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Ole Milya amezipongeza Ofisi ya Madini Mirerani, Tume ya Madini na watendaji wa Serikali mkoani Manyara kwa kazi wanayoifanya katika kusimamia sekta ya madini, huku akiwataka kutokata tamaa katika kutekeleza majukumu yao licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Habari Picha 20209

Amesema viongozi wa Serikali wapo tayari kushirikiana na watendaji hao kuhakikisha rasilimali za madini zinasimamiwa kwa ufanisi na kwa maslahi mapana ya Tanzania.

Ole Milya pia amemshukuru Waziri Mavunde kwa kufika Simanjiro na kutumia muda wake kusikiliza moja kwa moja kilio cha wananchi na wadau wa Tanzanite, akisema hatua hiyo imeonyesha umuhimu wa viongozi kuwafikia wananchi na kusikiliza changamoto zao.

“Kwa niaba ya wananchi wa Simanjiro, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja Simanjiro, kusikiliza wananchi na kuendelea kusimamia rasilimali za nchi yetu,” amesema Ole Milya.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali, viongozi, wachimbaji na wadau wengine wa sekta ya madini ni muhimu katika kuhakikisha Tanzanite inaendelea kuwa fahari ya Tanzania na chanzo kikubwa cha manufaa kwa wananchi na Taifa.

 

Mwisho….

Share This Article
Leave a Comment