Na Geofrwey Stephen
MIRERANI, SIMANJIRO —
wanaofanya kazi katika shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara, wameeleza namna ajira walizopata kupitia kampuni ya Franone Mining zilivyowasaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Wakizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, katika eneo la Mirerani, wanawake hao walimweleza Waziri Mavunde kuwa pamoja na changamoto ya uzalishaji wa madini kushuka, uongozi wa kampuni umeendelea kuwajali wafanyakazi na kuhakikisha wanapata mishahara yao kwa wakati.

Mmoja wa wanawake hao alimshukuru Waziri Mavunde kwa kuwatembelea na kusikiliza changamoto na mafanikio yao, akisema ajira wanazozipata kupitia shughuli za madini zimekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa familia zao.
Alisema kampuni hiyo imekuwa ikitoa ajira kwa watu mbalimbali katika jamii, huku ikiwapa wafanyakazi mazingira ya kufanya kazi bila unyanyasaji.
“Tunafanya kazi kwa uaminifu bila unyanyasaji wa aina yoyote. Pamoja na uzalishaji kuwa mdogo, tunapata mshahara wetu kwa wakati na hatujawahi kuteseka,” alisema mmoja wa wanawake hao.

Wanawake hao pia walitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sera na juhudi zake za kufungua fursa katika sekta ya madini, ambazo zimewezesha wananchi, wakiwemo wanawake wa Simanjiro, kushiriki katika shughuli za uchimbaji na kupata ajira.
Walimwomba Waziri Mavunde kufikisha salamu zao kwa Rais Samia, wakisema wanatambua mchango wa Serikali katika kukuza sekta ya madini na kuwezesha wananchi kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.
Waziri Mavunde aahidi kuongeza ufanisi.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema amefurahishwa kuona wanawake wakishiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji wa madini na kupata ajira kupitia mgodi huo.
Mavunde alisema sekta ya madini imeendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka migodi, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa tija zaidi.

Alisema pamoja na wanawake hao kueleza kuwa uzalishaji umepungua, jambo la msingi ni kuona wafanyakazi wanaendelea kupata mishahara na kampuni inaendelea kujali ustawi wao.
“Nimefurahi kusikia kwamba pamoja na uzalishaji sasa kwenda chini, bado mkurugenzi mkuu wa Franone anawajali na mshahara mnaupata vilevile,” alisema Mavunde.
Waziri huyo pia alieleza kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na uongozi wa kampuni pamoja na viongozi wa eneo hilo katika kutafuta njia za kuongeza ufanisi wa kazi zinazofanywa na wafanyakazi.
Alisema matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia kupunguza muda unaotumika katika baadhi ya shughuli za uchimbaji bila kuondoa ajira za wafanyakazi.

Kwa mujibu wa Mavunde, hatua hiyo inaweza kuwasaidia wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuongeza uzalishaji, huku wakibaki na ajira zao.
Teknolojia kusaidia shughuli za uchimbaji
Mavunde alisema Serikali itaendelea kuzungumza na viongozi wa eneo hilo na wadau wa sekta ya madini ili kuona namna teknolojia inavyoweza kutumika kuboresha shughuli za uchimbaji Mirerani.
Alisema lengo si kuondoa ajira za wananchi, bali ni kuwasaidia kufanya kazi kwa ufanisi na usalama zaidi.
“Bila kuondoa mshahara wenu, bila kuondoa kazi yenu, tunataka kuwasaidia namna ya kuongeza ufanisi wa kazi yenu,” alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia kupunguza muda unaotumika katika kazi ambazo kwa sasa zinafanywa kwa muda mrefu kwa kutumia nguvu kazi ya binadamu.
Franon Mining kuendelea kushirikiana na jamii.
Wanawake hao pia waliipongeza Franon Mining kwa kuwapa ajira watu mbalimbali na kuzingatia uwezo wa kila mfanyakazi katika kugawa majukumu.
Walisema ajira hizo zi
mekuwa na umuhimu mkubwa kwa jamii ya Mirerani kwa kuwa zinawawezesha wananchi kupata kipato na kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na sekta ya madini.

Waziri Mavunde aliahidi kuendelea kufuatilia maendeleo ya shughuli za madini katika eneo hilo na kushirikiana na viongozi wa Serikali, wabunge, viongozi wa chama na wadau wengine kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa wananchi.
Ziara hiyo pia ilitoa fursa kwa wanawake wanaofanya kazi katika shughuli za madini kueleza moja kwa moja kwa Serikali hali ya ajira zao, changamoto wanazokutana nazo na matarajio yao ya kuendelea kunufaika na rasilimali madini zilizopo Mirerani.

Wanawake hao walimaliza kwa kumshukuru Waziri Mavunde kwa kuwatembelea na kuwasikiliza, huku wakisisitiza umuhimu wa Serikali na wadau wa madini kuendelea kushirikiana ili shughuli za uchimbaji ziendelee na ajira walizonazo ziendelee kuwa chanzo cha kipato kwao na familia zao.

Mwisho.
