TAKUKURU Yamkamata Raia wa Romania kwa Tuhuma za Kutengeneza Kadi Bandia na Kutoa Fedha kwenye Akaunti za Watu

Geofrey Steven
2 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha:

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imemkamata raia wa Romania, Constantin Catalin Podoleanu (39), kwa tuhuma za kutengeneza kadi bandia za benki na kuzitumia kufanya miamala ya fedha kutoka kwenye akaunti za watu wengine.

Habari Picha 20087

Podoleanu alikamatwa Agosti 20, 2026, majira ya saa 4:00 usiku katika eneo la Njiro, Jijini Arusha. Baada ya kukamatwa, maafisa wa TAKUKURU walifanya upekuzi katika makazi yake yaliyopo Njiro Block D, Kata ya Engutoto, ambapo walikutwa na vifaa mbalimbali vinavyodaiwa kutumika katika shughuli hizo.

Habari Picha 20083
Habari Picha 20084

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amesema upekuzi huo ulifanikiwa kubaini vifaa kadhaa, ikiwemo mashine sita za POS, kadi mbalimbali za benki, kompyuta mpakato mbili, pamoja na vifaa na kemikali zinazodaiwa kutumika katika utengenezaji wa kadi bandia.

Fedha na stakabadhi zenye thamani kubwa zakutwa.

Mbali na vifaa hivyo, TAKUKURU imebaini pia fedha taslimu za Tanzania Sh milioni 2.17, fedha za kigeni pamoja na stakabadhi za malipo zenye thamani ya takribani Sh milioni 171.7 na Dola za Marekani 55,987.20.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, baadhi ya taarifa za kadi zilizodaiwa kutumika katika miamala hiyo zinahusishwa na raia wa mataifa mbalimbali nje ya Tanzania.

Inadaiwa kuwa fedha kutoka kwenye akaunti za watu hao zilitumika kulipia huduma mbalimbali nchini Tanzania, huku wahusika wenyewe wakidaiwa kutokuwa wamewahi kupata huduma hizo katika kipindi ambacho miamala hiyo ilifanyika.

Uchunguzi waendelea.

TAKUKURU Mkoa wa Arusha imeeleza kuwa inaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli, ukubwa wa mtandao huo na mazingira yote yanayohusiana na tuhuma hizo.

Habari Picha 20085
Habari Picha 20086

Taasisi hiyo imeongeza kuwa hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika, kwa mujibu wa sheria.

TAKUKURU imewataka wananchi kuwa makini na taarifa zao za kibenki na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapobaini miamala isiyo ya kawaida kwenye akaunti zao.

MWISHO..

Share This Article
Leave a Comment