ARUSHA KUTIKISA KIMATAIFA NOVEMBA: HORTILOGISTICA AFRICA 2026 YAIBUA FURSA KUBWA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI.

Geofrey Steven
4 Min Read

RC Makalla aahidi ushirikiano, ataka HortiLogistica Africa 2026 kuunganishwa na utalii na uchumi wa Arusha

ARUSHA, Tanzania —

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika kufanikisha Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji na Biashara la Horticulture, HortiLogistica Africa 2026, linalotarajiwa kufanyika mkoani Arusha mwezi Novemba mwaka huu.

Ahadi hiyo imetolewa Jumatatu, Agosti 10, 2026, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, baada ya Mhe. Makalla kupokea wasilisho rasmi kuhusu maandalizi ya jukwaa hilo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Taha Tanzania Horticultural Association . (TAHA), Dkt. Jackline Mkindi, aliyefika ofisini hapo akiwa ameambatana na ujumbe wake.

Habari Picha 19889
Habari Picha 19890

Jukwaa hilo linatarajiwa kufanyika Novemba 8 hadi 10, 2026, katika Ngurdoto Mountain Lodge, Arusha, likilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya mboga, matunda na maua kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.

Fursa za uwekezaji, biashara na teknolojia.

 

Kwa mujibu wa waandaaji, HortiLogistica Africa 2026 inalenga kuwa jukwaa muhimu la kimataifa la kukuza uwekezaji, biashara, teknolojia na masoko katika sekta ya horticulture.

Jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha wanunuzi wakubwa wa mazao, wazalishaji, wawekezaji, kampuni za teknolojia, kampuni za usafirishaji pamoja na taasisi za fedha kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Akizungumza baada ya kupokea wasilisho hilo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amesema tukio hilo lina umuhimu mkubwa kwa Arusha na Tanzania kwa ujumla kutokana na fursa pana za kiuchumi zinazoweza kuzalishwa kupitia sekta ya horticulture.

Habari Picha 19891

“Jambo hili linaipa heshima nchi yetu na Rais wetu kwa kuwaleta wadau wote wa mbogamboga, matunda na maua Arusha. Lakini pia ukitafuta tija ya jambo hili kiuchumi, mnyororo wake ni mkubwa. Kwa hiyo mimi kama Mkuu wa Mkoa, itoshe kusema kwamba sasa tunaanza safari pamoja ya kufanikisha jambo hili,” amesema CPA Makalla.

RC Makalla ataka jukwaa hilo kuunganishwa na utalii.

Mhe. Makalla pia amesisitiza umuhimu wa kulifungamanisha jukwaa hilo na sekta ya utalii pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi zinazofanyika mkoani Arusha.

Habari Picha 19898

Kwa mtazamo huo, HortiLogistica Africa 2026 siyo tu fursa kwa wadau wa horticultural  kukutana na kufanya biashara, bali pia ni nafasi ya kutangaza Arusha kama kitovu cha uwekezaji, utalii na biashara za kimataifa.

Arusha ikiwa ni moja ya maeneo muhimu ya utalii nchini Tanzania, kufanyika kwa jukwaa hilo kunatarajiwa kuongeza fursa za biashara kwa hoteli, usafirishaji, sekta ya huduma, biashara ndogo na za kati pamoja na wadau wengine wa uchumi wa mkoa.

TAHA: HortiLogistica kuwa jukwaa la kila mwaka.

Kwa upande wake, Dkt. Jackline Mkindi Mkurugenzi wa Asasi ya Sekta Binafsi Taha  amesema HortiLogistica Africa 2026 inalenga kuwa jukwaa la kimataifa litakalofanyika kila mwaka mkoani Arusha, likiwa sehemu ya kuunganisha wazalishaji na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Habari Picha 19894
Habari Picha 19893

Jukwaa hilo linatarajiwa kutoa nafasi kwa wadau kujadili fursa na changamoto zinazokabili sekta ya horticulture, pamoja na kuibua mikakati ya kuongeza uzalishaji, uwekezaji, biashara, teknolojia na upatikanaji wa masoko ya kimataifa.

Kwa kufanyika kwake Arusha, HortiLogistica Africa 2026 inatarajiwa kuwa moja ya matukio muhimu ya kimataifa yatakayoiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi katika ramani ya biashara na uwekezaji kwenye sekta ya mboga, matunda na maua barani Afrika.

Habari Picha 19896
Habari Picha 19895

HortiLogistica Africa 2026 inatarajiwa kufanyika Novemba 8–10, 2026, katika Ngurdoto Mountain Lodge, Arusha.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment