Na Geofrey Stephen Arusha
Halmashauri ya Jiji la Arusha imeidhinisha uwekezaji wa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kufunga zaidi ya taa 500 za barabarani, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa wananchi, kukuza biashara za usiku na kuifanya Arusha kuwa jiji linalofanya shughuli za kiuchumi kwa saa 24.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Meya wa Jiji la Arusha, alisema kuwa Halmashauri imeendelea kutekeleza sera ya kuelekeza asilimia 60 ya mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.
Bilioni 61 Zakadiriwa Kukusanywa.
Meya Iranghe alieleza kuwa katika mwaka wa fedha husika, Jiji la Arusha linatarajia kukusanya shilingi bilioni 61 kupitia mapato ya ndani. Baada ya makato ya kisheria, fedha zilizobaki zitaelekezwa moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wake, mradi wa taa za barabarani utatekelezwa katika kata mbalimbali za jiji, ikiwemo kuboresha maeneo ambayo tayari yana miundombinu ya taa kama Livolosi, Kaloleni na Sekei, ili kuongeza usalama na kuimarisha mazingira ya biashara.
Kodi za Wananchi Zinaonekana Kwa Vitendo.
Meya huyo alisisitiza kuwa fedha zinazotumika ni kodi za wananchi, hivyo Halmashauri ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanaona matokeo ya michango yao kupitia miradi inayoboresha huduma na miundombinu.
Alibainisha kuwa pamoja na mradi wa taa, Jiji linaendelea kunufaika na miradi ya ujenzi wa barabara inayotekelezwa na Serikali Kuu. Aidha, Halmashauri imeanza mchakato wa utekelezaji wa zabuni za miradi mipya ya barabara za ndani, mitaro ya maji ya mvua, madaraja madogo na vivuko kwa lengo la kupunguza changamoto za usafiri na mafuriko.
Bilioni 9.2 Zinatarajiwa Kukusanywa Kupitia Mawakala.
Katika hatua nyingine, Halmashauri imesaini mikataba na mawakala wa ukusanyaji wa madeni pamoja na ushuru wa maegesho (parking), ambapo zaidi ya shilingi bilioni 9.2 zinatarajiwa kukusanywa kupitia mfumo huo.
Meya aliwataka mawakala hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na kwa kuzingatia masharti ya mikataba waliyoingia nayo, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayewatoza wananchi kinyume cha sheria au kushindwa kutekeleza wajibu wake.
“Mawakala wakifanya vizuri wataendelea na kazi, lakini wakishindwa kutekeleza wajibu wao au kukiuka taratibu, mkataba unaweza kusimamishwa wakati wowote,” alisema Meya Iranghe.
Wananchi Wahimizwa Kulipa Kodi Kidijitali
Aidha, wananchi wamehimizwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari kupitia mifumo ya kidijitali ikiwemo simu za mkononi na benki. Meya alisema maboresho ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato yameongeza uwazi na kupunguza migogoro kati ya walipakodi na mawakala.
Aliongeza kuwa Halmashauri itaendelea kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuongeza uwazi na kuwajengea wananchi imani kuwa mapato yao yanatumika kuboresha huduma za jamii na miundombinu ya Jiji la Arusha.
Arusha Yaendelea Kuelekea Uchumi wa Saa 24.
Uwekezaji wa bilioni mbili katika taa za barabarani unaonekana kuwa hatua muhimu katika mkakati wa kuifanya Arusha kuwa jiji salama, lenye mazingira bora ya uwekezaji na biashara zinazofanyika saa 24, huku maendeleo ya miundombinu na mifumo ya ukusanyaji wa mapato yakipewa kipaumbele kwa manufaa ya wananchi wote.
Mwisho.
