Na Geofrey Stephen ARUSHA, Agosti 4, 2026
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Lameck Karanga, amewahimiza wakulima na wafanyabiashara kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na sekta ya utalii kwa kuunganisha uzalishaji wa mazao ya kilimo na mahitaji ya mahoteli pamoja na watalii wanaotembelea Mkoa wa Arusha.


Akizungumza leo Jumanne, Agosti 4, 2026, katika Viwanja vya Themi Njiro jijini Arusha wakati wa Maonesho ya Wakulima na Wafugaji na maadhimisho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini, Mhe. Karanga alisema sekta ya utalii imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha soko la mazao ya wakulima na fursa ya kuongeza kipato kwa wananchi.
Mhe. Karanga amesema Wilaya ya Karatu ina zaidi ya hoteli 300 zenye viwango mbalimbali kuanzia nyota moja hadi saba, ambazo zinahitaji bidhaa mbalimbali za kilimo zinazozalishwa na wakulima wa ndani kwa ajili ya kuhudumia maelfu ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii kama Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa Serengeti.
“Karatu ina fursa kubwa sana ya kiuchumi kupitia utalii. Wageni wanaokuja hapa wanahitaji chakula na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wakulima wetu. Wakulima watumie nafasi hii kupeleka mazao yao kwenye hoteli na kujiongezea kipato,” amesema Mhe. Karanga.


Ameeleza kuwa msimu wa utalii (high season) unaoendelea hadi mwezi Oktoba ni kipindi muhimu kwa wakulima wa Karatu pamoja na wale wa mikoa jirani ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kwa kuzalisha mazao yenye ubora na yanayokidhi mahitaji ya soko.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, mazao kama mboga za majani, matunda, maboga na mazao mengine ya bustani yanahitajika kwa wingi na mahoteli pamoja na kambi za watalii, jambo linalowapa wakulima soko la uhakika na kuongeza thamani ya uzalishaji wao.
“Sisi tuna hoteli zaidi ya mia tatu. Wageni wetu wanatumia bidhaa zinazopatikana hapa, ikiwemo mboga za majani, maboga na mazao mengine. Tunawaomba wakulima walete bidhaa zao ili ziweze kufika moja kwa moja kwa watalii na kwenye mahoteli,” amesisitiza.


Katika hatua nyingine, Mhe. Karanga amewapongeza wajasiriamali wanaozalisha kahawa kwa kutumia chapa ya utalii ya Tanzania ya ‘Big Five’ kutangaza bidhaa zao, akisema ubunifu huo unaongeza thamani ya bidhaa, unaimarisha ushindani wake katika soko la kimataifa na kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia bidhaa za ndani.
Amesema ushirikiano kati ya sekta ya kilimo na utalii ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa wananchi, kuongeza ajira na kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika kwa mazao yao mwaka mzima.


Mwisho.
