Na Geofrey Stephen Arusha
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (APSP), Dkt. Emmanuel Urembo, amesema mustakabali wa taaluma ya ununuzi na ugavi unategemea uwezo wa wataalamu kuendana na mabadiliko ya teknolojia, kuzingatia maadili na kuwa washauri wa kimkakati wanaochangia maendeleo ya taasisi na taifa.
Akizungumza katika mkutano Mkuu wa Tano wa wanachama wa APSP uliofanyika Arusha katika ukumbi wa mikutano wa AICC Bwayuwayu, Dkt. Urembo alisema taaluma ya ununuzi imebadilika na haihusiani tena na kutoa oda, kupokea bidhaa au kulipa ankara pekee, bali ni mchakato unaohakikisha taasisi zinapata bidhaa, huduma na kazi kwa ubora unaotakiwa, kwa wakati na kwa gharama zinazotoa thamani ya fedha.


“Mtaalamu wa ununuzi na ugavi wa leo hawezi kuwa msimamizi wa sheria pekee; anapaswa kuwa mshauri wa kimkakati anayeelewa soko, gharama, teknolojia, usimamizi wa hatari na mzunguko wa maisha wa mali na miradi,” alisema.
Alieleza kuwa kaulimbiu ya mkutano inayohusu kuimarisha ushiriki wa taaluma, kuwezesha makundi maalumu ya biashara ndogo na za kati kunufaika na urasimishaji wa biashara, umiliki halisi (Beneficial Ownership) na fursa za ununuzi wa umma, inalenga kuhakikisha wataalamu wanakuwa kiungo kati ya sheria na utekelezaji wa maendeleo.
Kwa mujibu wa Dkt. Urembo, mafanikio ya mtaalamu wa ununuzi hayapimwi kwa idadi ya zabuni zilizotolewa au bidhaa zilizonunuliwa, bali kwa kiwango ambacho taasisi imepata thamani ya fedha na kufikia malengo yake ya maendeleo.

Katika hotuba yake, aliwahimiza wanachama kuweka mkazo katika maandalizi ya bajeti za ununuzi zinazozingatia mahitaji halisi, kuimarisha uwazi na ushindani katika michakato ya ununuzi, kutumia kikamilifu mifumo ya kidijitali kama NeST na kuboresha usimamizi wa mikataba ili kuhakikisha utekelezaji wake unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Dkt. Urembo pia alieleza kuwa APSP inaendelea kukua na kuimarika ikiwa na wanachama zaidi ya 2,200 kutoka sekta za umma na binafsi.

Alitaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa sasa kuwa ni pamoja na kusaini hati ya makubaliano na taasisi mbalimbali, kukamilisha ulipaji wa deni la kiwanja cha chama lenye thamani ya shilingi milioni 134, kusajili nembo ya APSP kupitia BRELA, kukamilisha ukaguzi wa hesabu za chama kwa miaka miwili mfululizo na kuendelea kutoa mafunzo ya kitaaluma kwa wanachama.
Alisema mafanikio hayo yanaonyesha kuwa chama kinaendelea kujenga msingi imara wa kitaaluma na kitaasisi, huku akiwataka wanachama kuendelea kujifunza na kuzingatia maadili ya taaluma.

Naye Mlezi Mkuu wa APSP, Dkt. Frederick A. Mwakibinga, aliwapongeza viongozi na wanachama kwa hatua walizofikia tangu kuanzishwa kwa chama mwaka 2020, akisema mafanikio hayo yanaashiria kuwa APSP imevuka hatua ya kujijenga na sasa inaelekea kuwa taasisi yenye mifumo imara na mchango mkubwa katika maendeleo ya taaluma ya ununuzi nchini.
Alisema taaluma hiyo imekuwa sehemu ya maisha yake kwa zaidi ya miaka 39 aliyohudumu katika utumishi wa umma.
“Nimefanya kazi miaka 39 na miezi sita katika eneo hili. Ukinitaja ununuzi na ugavi, moyo wangu unaamka. Hata familia yangu wakiona taarifa yoyote inayohusu taaluma hii hunitaarifu mara moja. Naamini ni kifo pekee kitakachonitenganisha na taaluma hii,” alisema.

Mlezi huyo alisema amepitia taarifa ya maendeleo ya chama na kujionea mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo kuimarika kwa uwajibikaji wa kifedha kupitia ukaguzi wa hesabu, ushirikiano na taasisi mbalimbali pamoja na mchango wa APSP katika kutafsiri mfumo wa NeST kwa lugha ya Kiswahili.
Alisema hatua hizo zinaonyesha dhamira ya viongozi na wanachama kujenga taasisi yenye misingi imara licha ya majukumu makubwa waliyonayo katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, alisema amefurahishwa kuona wataalamu wa ununuzi na ugavi wakianza kutambuliwa kama wafanyakazi bora katika taasisi mbalimbali za serikali, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo taaluma hiyo mara nyingi ilihusishwa na lawama.
“Kwa miaka mingi tulizoea kusikia lawama zikielekezwa kwa wataalamu wa ununuzi. Leo tunaanza kuona wakitajwa kama wafanyakazi bora. Hii ni ishara kwamba taswira ya taaluma inaanza kubadilika,” alisema.
Aliwataka wataalamu hao kuendelea kulinda heshima ya taaluma kwa kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi na weledi, akisisitiza kuwa viongozi huwa tayari kuwaunga mkono watumishi wanaojituma na kuonyesha matokeo mazuri.
“Tuanze kwa kuonyesha umahiri wetu na uadilifu wetu. Tukifanya hivyo, itakuwa rahisi kupata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi na wadau mbalimbali. Heshima ya taaluma inaanzia kwenye matendo yetu wenyewe,” alisisitiza.
Kwa pamoja, viongozi hao walitoa wito kwa wanachama wa APSP kuendelea kuimarisha taaluma ya ununuzi na ugavi kwa kuzingatia sheria, maadili na matumizi ya teknolojia, wakisema sekta hiyo ina nafasi muhimu katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na wananchi wanapata huduma bora.
Mwisho.
