Hai, Kilimanjaro –
Julai 18, 2026
Wananchi wa Kitongoji cha Mungushi Kati, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro,
wameonesha mshikamano kwa kuanza ukarabati wa nyumba ya mkazi mwenzao, Merry Muro, ambaye nyumba yake iliteketea kwa moto pamoja na mali zote zilizokuwemo ndani. Katika tukio hilo, watoto wawili walijeruhiwa na wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya KCMC.

Akizungumza leo Julai 18, 2026, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mungushi Kati, Joachim Mbowe, wakati wa kutembelea maendeleo ya ukarabati huo, alisema wananchi waliguswa na tukio hilo na kuamua kuchangishana fedha ili kumsaidia mwathirika huyo kurejea katika makazi yake.
Mbowe alisema mara baada ya tukio hilo, ambalo linadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme, aliiitisha mkutano wa dharura wa wananchi kujadili namna ya kumsaidia Merry Muro.
“Baada ya nyumba kuungua na mali mbalimbali kuteketea, ikiwemo televisheni, magodoro, nguo na vyakula, tuliitisha mkutano wa dharura. Wananchi waliitikia wito na kupitisha mchango wa ukarabati wa nyumba, kwani mwenzetu alikuwa amelazimika kulala nje,” alisema Mbowe.

Alieleza kuwa utaratibu wa kusaidiana wakati wa majanga ni sehemu ya utamaduni waliojiwekea katika kitongoji hicho, akisema unajenga upendo, mshikamano na kuwapa faraja wanaopatwa na matatizo.
Mbowe pia alisema Mbunge wa Jimbo hilo, Saashisha Mafuwe, alichangia mabati 10 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba hiyo, akimpongeza kwa moyo wa kujitolea na kuwajali wananchi wake.
Aidha, aliwashukuru wadau wa maendeleo wa Light African kwa kugharamia matibabu ya watoto wawili waliojeruhiwa katika ajali hiyo ya moto. Watoto hao wenye umri wa miaka miwili na saba wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya KCMC.
Kwa upande wake, Merry Muro alisema tukio hilo lilitokea mchana wa Julai 14, 2026, na kusababisha kupoteza nyumba pamoja na mali zote zilizokuwemo ndani. Aliwashukuru wananchi wa Kitongoji cha Mungushi Kati na kijiji kwa ujumla kwa kujitokeza haraka kuokoa watoto waliokuwa ndani ya nyumba wakati moto ulipozuka.

Alisema anafarijika kuona wananchi hao hao wameendelea kumuunga mkono kwa michango ya fedha na vifaa vya ujenzi ili nyumba yake ikarabatiwe na aweze kurejea kuishi humo. Aliwaomba waendelee kudumisha moyo huo wa kusaidiana.
Naye mkazi wa Bomang’ombe, Wilaya ya Hai, Juma Ramadhani, amepongeza hatua ya wananchi wa Mungushi Kati, akisema ni mfano wa kuigwa. Aliwataka wananchi wa maeneo mengine kuendeleza utamaduni wa kusaidiana wakati wa majanga, akieleza kuwa jambo hilo linaimarisha umoja na mshikamano katika jamii.
Mwisho

