Na Geofrey Stephen .Arusha
Naibu Waziri Zainab Katimba asema mawakili wa serikali wanapaswa kuwa viongozi wa kimkakati katika kusukuma Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika ujenzi wa uwezo na matumizi ya teknolojia.
Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuimarisha taaluma ya uwakili wa serikali kwa kuwekeza katika mafunzo, teknolojia na uongozi wa kimkakati ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za kisheria na kulinda maslahi ya umma.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, wakati akifunga Mafunzo ya Tatu ya BSPOC kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), yakihusisha mawakili wa serikali kutoka wizara, idara zinazojitegemea, wakala, mamlaka za serikali za mitaa, mashirika ya umma na vyuo vikuu.
Katimba aliipongeza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kuandaa mafunzo yanayolenga kujenga uwezo wa mawakili wa serikali ili waendane na mabadiliko ya mazingira ya utoaji wa huduma za kisheria.
“Leo hii wakili wa serikali hatarajiwi kuwa mtaalamu wa kutafsiri sheria pekee, bali awe kiongozi anayeshiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi makubwa ya taasisi na serikali kwa ujumla kwa kutoa ushauri wa kitaalamu na wa kimkakati.”
Aidha, alimpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, pamoja na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samweli Maneno, kwa kuendeleza programu hiyo ambayo sasa imefanyika kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Katika hotuba yake, Katimba alieleza kuwa Serikali imeongeza nguvu katika uwekezaji wa maendeleo ya kitaaluma kwa mawakili wa serikali ili kuhakikisha wanaendelea kukabiliana na changamoto za karne ya 21.
Akizungumza kuhusu uwekezaji huo, alisema taarifa iliyowasilishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaonesha kuwa Serikali imetenga shilingi bilioni 6.6 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya mawakili wa serikali nchini.
“Hii ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha mawakili wa serikali wanaendelea kujengewa uwezo bila kubebeshwa gharama za mafunzo, ili waendelee kutoa huduma bora kwa taifa.”
Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samweli Maneno, akiwasilisha taarifa ya mafunzo hayo mbele ya mgeni rasmi, alisema washiriki walipata mafunzo yaliyolenga kuwaandaa kukabiliana na mazingira mapya ya utoaji wa huduma za kisheria katika taasisi za umma.

Alisema mada zilizowasilishwa zilihusu usimamizi wa majadiliano na mikataba ya kimkakati, usuluhishi wa migogoro, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), usimamizi wa vihatarishi vya kisheria (Legal Risk Management), pamoja na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence) katika taaluma ya sheria.

Washiriki pia walijengewa uwezo kuhusu makosa ya mtandao, mawasiliano ya umma, jiografia ya kisiasa (Geopolitics) na siasa za kimataifa ili kuwawezesha kutoa ushauri wa kisheria unaozingatia mazingira ya sasa ya dunia.
Maneno alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za Preventive Legal Services kupitia matumizi ya teknolojia kwa kuboresha mfumo wa kisasa wa usimamizi wa taarifa na mikataba ya serikali.
“Lengo letu ni kuhakikisha huduma za kinga za kisheria zinatolewa kwa wakati kwa kutumia teknolojia, huku mawakili wa serikali wakishiriki kikamilifu katika maamuzi yote muhimu ya taasisi tangu hatua za awali.”
Aliongeza kuwa kuanzia sasa mikataba ya serikali itaendelea kusimamiwa kupitia mifumo ya kielektroniki ili kuongeza uwazi, ufanisi na usimamizi bora wa mikataba ya umma.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliongozwa na kaulimbiu isemayo, “Repositioning State Attorneys for Strategic Legal Leadership in Realizing Tanzania Development Vision 2050,” ambayo imeweka msisitizo kwa mawakili wa serikali kuwa viongozi wa kimkakati katika kusimamia utawala wa sheria, kulinda rasilimali za umma na kuchangia kikamilifu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mwisho..
