Zanzibar Yaongeza Kasi ya Kuimarisha Umahiri wa Madereva Kupitia Ushirikiano na Chuo cha Ufundi Arusha

Geofrey Steven
5 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

Mafunzo ya kisasa ya udereva, matumizi ya teknolojia na ujenzi wa uwezo wa walimu wa vyuo vya udereva yamepewa kipaumbele katika jitihada za kuboresha usalama barabarani nchini.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Bandria Masoud, ametembelea Chuo cha Ufundi Arusha kwa lengo la kujionea kwa karibu namna taasisi hiyo inavyotoa mafunzo ya umahiri wa madereva na kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya sekta ya usafiri na uchukuzi.

Mhe. Masoud, ambaye alimwakilisha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salim Muhammad, alisema ziara hiyo imekuwa ya manufaa makubwa licha ya kuwa ya muda mfupi, kwani imempa fursa ya kujifunza mifumo mbalimbali inayotumika katika mafunzo ya madereva na teknolojia za kisasa za magari.

Alieleza kuwa Zanzibar ipo katika kipindi cha mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya ujenzi na uchukuzi, hivyo uzoefu uliopatikana katika ziara hiyo utasaidia kuimarisha maboresho yanayoendelea.

“Ninaondoka nikiwa nimejifunza mambo mengi muhimu yatakayosaidia kuendeleza maboresho ya sekta ya uchukuzi Zanzibar. Tumeona mifumo mizuri ya mafunzo na matumizi ya teknolojia ambayo inaweza kutusaidia kujenga mfumo imara wa mafunzo ya madereva,” alisema Mhe. Masoud.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Zanzibar ulipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya chuo, ikiwemo madarasa, karakana na maabara za mafunzo, ambapo walijionea namna wanafunzi wanavyopatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu uendeshaji salama wa magari, ukaguzi wa magari kabla ya safari na utambuzi wa hitilafu.

Wakufunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha walieleza kuwa mafunzo hayo yamezingatia mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya magari, ambapo wanafunzi hufundishwa matumizi ya magari yenye gia za kawaida (manual transmission) pamoja na magari yenye gia otomatiki (automatic transmission), sambamba na uelewa wa mifumo mbalimbali ya magari ya kisasa.

Aidha, ujumbe huo ulipata maelezo kuhusu magari ya dizeli yenye mfumo wa Common Rail, matumizi ya viashiria vya dashibodi kama Check Engine, pamoja na namna vifaa vya uchunguzi wa hitilafu (diagnostic systems) vinavyotumia kompyuta vinavyosaidia kubaini matatizo ya magari kwa usahihi.

Chuo cha Ufundi Arusha na Zanzibar waimarisha mafunzo ya udereva

Akizungumzia ushirikiano huo, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Profesa Musa Chacha, alisema Tanzania imeendelea kuimarisha mafunzo ya udereva baada ya kubaini kuwa changamoto ya ajali za barabarani haihusiani na uzembe pekee, bali pia inatokana na upungufu wa maarifa na ujuzi wa baadhi ya madereva.

“Tumeweza kubaini kuwa Tanzania bado inahitaji kuimarisha zaidi mafunzo ya udereva. Kwa muda mrefu imekuwa ikionekana kuwa ajali nyingi husababishwa na uzembe wa madereva, lakini kwa mtazamo wetu changamoto kubwa ni ukosefu wa mafunzo ya kutosha yanayowawezesha madereva kuelewa kwa kina wajibu wao na mazingira ya uendeshaji salama barabarani,” alisema Prof. Chacha.

Alisema hatua ya kwanza iliyochukuliwa na chuo hicho ilikuwa kuwajengea uwezo walimu wa vyuo vya udereva ili waweze kutoa mafunzo yenye viwango vya kitaalamu kwa madereva nchini.

Kwa mujibu wa Prof. Chacha, baada ya kuona mafanikio ya mpango huo, Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar iliwasiliana na Chuo cha Ufundi Arusha kuomba ushirikiano wa kuanzisha mafunzo hayo Zanzibar.

Ushirikiano huo ulianza kutekelezwa kwa kushirikiana na Karume Institute of Science and Technology (KIST), ambapo wakufunzi kutoka Chuo cha Ufundi Arusha wamekuwa wakitoa mafunzo kwa walimu wa vyuo vya udereva Zanzibar ili kuwawezesha kutoa elimu bora kwa madereva.

Prof. Chacha alisema ushirikiano huo umefanikiwa kutokana na mshikamano kati ya Chuo cha Ufundi Arusha, Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa ushiriki wa Mhe. Bandria Masoud katika uzinduzi wa mafunzo hayo Zanzibar unaonesha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha sekta ya uchukuzi na kuandaa madereva wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa.

Baada ya ziara yake Chuo cha Ufundi Arusha, Mhe. Masoud alieleza kuridhishwa na kiwango cha mafunzo yanayotolewa na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na chuo hicho.

Kupitia ushirikiano huo, Zanzibar itaendelea kupeleka walimu wa vyuo vya udereva na wadau wa sekta ya uchukuzi kupata mafunzo ya kitaalamu, huku ikiimarisha programu za mafunzo ya udereva visiwani.

Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza umahiri wa walimu na madereva, kuboresha usalama barabarani na kuandaa rasilimali watu wenye weledi unaokidhi mahitaji ya sekta ya usafiri na uchukuzi nchini.

 

Mwisho

Share This Article
Leave a Comment