Na Geofrey Stephen Arusha .
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Alnason Nguvila, ametunukiwa Tuzo ya Heshima na Halmashauri ya Jiji la Arusha, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuimarisha utendaji kazi na misingi ya utumishi bora wa umma.
Dkt. Toba alipokea tuzo hiyo muda mfupi baada ya kufungua kikao kazi cha Watendaji wa Serikali Mkoa wa Arusha kinachoendelea katika Hoteli ya Masai Land, Wilaya ya Arumeru, asubuhi ya leo Julai 17, 2026.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya tuzo hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Shan Ferdinand Manyama, amesema utambuzi huo umetolewa kutokana na mchango mkubwa wa Dkt. Toba katika kusimamia na kuimarisha uwajibikaji, nidhamu na ufanisi katika utumishi wa umma.
Amesema uongozi wa Dkt. Toba umeendelea kuwa chachu katika kuhamasisha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kujikita katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Tuzo hiyo imepokelewa kama alama ya kuthamini juhudi za viongozi wanaoweka mbele maslahi ya umma na kuhakikisha mifumo ya utendaji inaimarishwa kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla.

Hongera sana Dkt. Toba Alnason Nguvila kwa kutambuliwa kwa kazi yako njema. Tuzo hii ni kielelezo cha utii, uzalendo, kujituma na uwajibikaji wenye tija katika kuwatumikia watumishi na wananchi.

