Na Geofrey Stephen Arusha:
Mawakili wa Serikali wametakiwa kutumia taaluma ya sheria kama nyenzo muhimu ya kuongoza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha mifumo ya sheria inaendana na mahitaji ya maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa Awamu ya Tatu ya Mafunzo ya Mawakili wa Serikali na Washauri wa Sheria katika Utumishi wa Umma yanayofanyika jijini Arusha.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali ili wawe viongozi wa kimkakati katika kutoa ushauri wa kisheria na kusimamia utekelezaji wa sera na sheria zinazochochea maendeleo ya Taifa.
Mafunzo Yalenga Kuimarisha Uwezo wa Kitaaluma.
Akiwasilisha utangulizi wa mafunzo hayo, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw. Onorious Njole, alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mpango wa kujenga uwezo wa Mawakili wa Serikali ulioanza miaka miwili iliyopita.

Alieleza kuwa mafunzo ya siku tatu yameandaliwa katika maeneo makuu matatu yenye mada 11 zinazolenga kuimarisha uelewa, kuongeza ubora wa kitaaluma na kuwezesha kubadilishana uzoefu miongoni mwa wataalamu wa sheria serikalini.
“Mada hizi zimejikita katika kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali kutumia mifumo na nyenzo za kisheria kuongoza na kuweka msingi madhubuti wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema Bw. Njole.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yamevutia zaidi ya washiriki 650, idadi inayokaribia 700, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita. Hali hiyo inaashiria kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo katika kuboresha utendaji wa Mawakili wa Serikali.
Sheria Ziwe Chachu ya Maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mratibu wa Ushauri wa Sheria, Bi. Neema Njole alisema maelekezo ya Rais ya kupitia upya sheria zote za nchi yanaweka wajibu mkubwa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Kurekebisha Sheria na Mawakili wa Serikali kuhakikisha sheria zinaendana na mahitaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema Mawakili wa Serikali wana nafasi muhimu katika kuhakikisha sheria zinazoandaliwa, kutafsiriwa na kutekelezwa zinaunga mkono ajenda ya maendeleo ya Taifa.


“Sisi kama Mawakili wa Serikali ni sehemu ya safari ya utekelezaji wa maelekezo hayo. Tunapaswa kuhakikisha sheria zinazotumika zinawezesha kufikiwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema Bi. Genzi.
Aidha, alisema kaulimbiu ya mafunzo hayo, “Repositioning State Attorneys for Strategic Legal Leadership in Realizing Tanzania Development Vision 2050,” inalenga kuwawezesha Mawakili wa Serikali kuwa viongozi wa kimkakati katika kutoa ushauri wa kisheria na kusimamia masuala muhimu ya maendeleo.
Miongoni mwa mada zinazojadiliwa ni uongozi wa kimkakati, usimamizi wa mikataba, utatuzi wa migogoro, uwekezaji, usimamizi wa hatari za kisheria pamoja na sheria na teknolojia.
Mwanasheria Mkuu: Sheria Ni Daraja la Kufikia Dira ya 2050.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Hamza Johari, alisema Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo Mawakili wa Serikali wanapaswa kutambua nafasi yao muhimu katika safari hiyo.
Alisema dira hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu ifikapo mwaka 2050, wenye ushindani, ujumuishi na ustahimilivu unaoboresha maisha ya wananchi.

“Tunapaswa kuhakikisha sheria zetu zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Sheria hizo zinapaswa kuwa daraja litakalowezesha Taifa kufikia malengo yake. Kwa maana nyingine, sisi Mawakili wa Serikali ni sehemu ya daraja hilo,” alisema Dkt. Johari.
Alisisitiza pia umuhimu wa mabadiliko ya mtazamo kwa Mawakili wa Serikali ili wawe viongozi wa kimkakati wanaotumia taaluma yao kuchochea maendeleo ya Taifa.
Hitimisho.
Dkt. Johari aliwahimiza washiriki kutumia mafunzo hayo kuongeza maarifa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wao wa kutekeleza majukumu kwa ubunifu, weledi na ufanisi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamewakutanisha Mawakili wa Serikali, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na viongozi kutoka wizara, taasisi za umma na ofisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kitaaluma na kuhakikisha sheria zinaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya Taifa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mwisho…
