Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yatategemea uwepo wa mfumo imara wa sheria, taasisi zenye uwezo pamoja na mikataba yenye tija inayolinda maslahi ya Taifa na rasilimali zake.
Rais Samia alitoa kauli hiyo Julai 13, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), akisisitiza kuwa sekta ya sheria ina nafasi ya msingi katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya nchi.

Alisema mawakili na maafisa wa sheria wa Serikali wanapaswa kuhakikisha mifumo ya kisheria inaendana na mahitaji ya sasa ya maendeleo pamoja na malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Ili kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaoongozwa na maarifa na ubunifu, ni lazima tuwe na mfumo wa sheria unaolinda maslahi ya Taifa na unaokwenda sambamba na mabadiliko ya wakati,” alisema Rais Samia.
Rais alieleza kuwa mageuzi ya uchumi wa dunia na kasi ya maendeleo ya teknolojia yameifanya Tanzania kuwa na wajibu wa kuendelea kuboresha sheria na sera zake ili ziweze kukidhi mahitaji ya mazingira ya sasa.
Alitaja maeneo yanayohitaji umakini mkubwa kuwa ni pamoja na uchumi wa kidijitali, ulinzi wa taarifa na data, usimamizi wa rasilimali za madini, bandari na ardhi, biashara za kikanda pamoja na ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa Rais, uwepo wa sheria zinazotabirika na mazingira rafiki ya kisheria utasaidia kuongeza ushindani wa Taifa, kuvutia uwekezaji wenye manufaa na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumzia mabadiliko yanayoendelea katika sera za kiuchumi na kisiasa duniani, Rais Samia alisema wataalamu wa sheria wanapaswa kuendelea kusimamia kwa weledi mikataba, sheria na taratibu mbalimbali ili kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanalindwa wakati wote.
Alisisitiza kuwa ulinzi wa uchumi wa Taifa, rasilimali za nchi na uwekezaji unapaswa kupewa kipaumbele kupitia usimamizi makini wa sheria na mikataba ya maendeleo.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Nchi alizitaka taasisi zote za umma kuimarisha mifumo ya kubaini na kudhibiti vihatarishi vya kisheria mapema ili kupunguza migogoro na hasara zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Alibainisha kuwa maeneo yanayohitaji uangalizi zaidi ni mikataba ya Serikali,manunuzi ya umma, miradi ya maendeleo, usimamizi wa ardhi, TEHAMA, mazingira pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, aliwataka mawakili wa Serikali kuendelea kusimamia utungaji na utekelezaji wa sheria zinazolinda uhuru wa Taifa, haki za wananchi na rasilimali za umma, huku wakidumisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na haki.

Kauli za Rais Samia zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatekelezwa katika mazingira ya utawala wa sheria, uwazi na taasisi zenye nguvu. Wadau wa sekta ya sheria wanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya safari hiyo kwa kuhakikisha mifumo ya kisheria inaendelea kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yanayoikabili Tanzania na dunia kwa ujumla.
Mwisho.

