ULEGA SERIKALI YATOA MWELEKEO MPYA: BARABARA ZA ARUSHA KM 70 ZIHARAKISHWE KABLA YA AFCON 2027”

Geofrey Steven
5 Min Read

Na Geofrey Stephen ,Arusha

Serikali imeitaka kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kuongeza kasi ya ujenzi wa mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 70 katika Jiji la Arusha, huku ikiweka mkazo maalum kwa sehemu ya kilomita 13 zinazohusishwa na maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameiagiza kampuni hiyo kufanya kazi kwa kasi kubwa kwa kuongeza mitambo, wataalamu na wafanyakazi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Habari Picha 19010

Ulega alitoa maagizo hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kupokea taarifa ya utekelezaji kutoka kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Masawe.

Akizungumza na wananchi wa Kiseriani na Kwa Mrombo, Waziri Ulega alisema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Habari Picha 19011
Habari Picha 19012

“Rais anawapenda sana wananchi wa Arusha na amenituma niwaletee salamu zake za upendo. Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema Ulega.

Mradi wa Km 70 Kuunganisha Maeneo Muhimu Arusha.

Mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha mtandao wa barabara ndani ya Jiji la Arusha na unalenga kuunganisha maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo Mbauda, Kwa Mrombo, Barabara ya Bypass, Soko la Kilombero, Kisongo hadi maeneo yanayohusiana na maandalizi ya AFCON 2027.

Habari Picha 19014
Habari Picha 19013

Waziri Ulega alisisitiza kuwa mkandarasi anatakiwa kuhakikisha kazi zinaendelea katika maeneo yote kwa wakati mmoja badala ya kuhamisha vifaa kutoka eneo moja kwenda jingine.

“Kila sehemu ya mradi iwe na vifaa vyake, wataalamu wake na wafanyakazi wake. Kazi zifanyike kwa wakati mmoja katika maeneo yote. Ongezeni mitambo, ongezeni wafanyakazi na hakikisheni mnafanya kazi mchana na usiku ili mradi ukamilike kwa wakati,” alisema.
Aidha, alisema Serikali haitakubali kazi zisizo na viwango, akieleza kuwa fedha zinazotumika ni za wananchi hivyo wanapaswa kupata miundombinu imara na yenye ubora wa kudumu.

Kilomita 13 Za AFCON 2027 Zapewe Kipaumbele.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Masawe, alisema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 221 unahusisha ujenzi wa kilomita 70, ambapo kilomita 55 zipo Mkoa wa Arusha na kilomita 15 zipo Mkoa wa Manyara.

Alisema mkataba wa mradi ulianza kutekelezwa rasmi Aprili 10, 2026 baada ya mkandarasi kupokea malipo ya awali na kupewa ruhusa ya kuanza kazi.

Habari Picha 19015

Mradi mzima unatarajiwa kukamilika Machi 25, 2029, lakini Serikali imeelekeza nguvu kubwa katika kukamilisha kilomita 13 muhimu kabla ya Januari 2027 ili kuwezesha maandalizi na ukaguzi wa miundombinu kwa ajili ya AFCON 2027.

“Mkazo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kilomita 13 zinazohusiana na maandalizi ya AFCON zinakamilika kabla ya Januari 2027,” alisema Mhandisi Masawe.

Barabara Yenye Viwango vya Kisasa.

Kwa mujibu wa TANROADS, barabara hiyo itajengwa kwa viwango vya kisasa ikiwa na njia za watembea kwa miguu, mifereji ya maji, taa za barabarani katika maeneo muhimu pamoja na miundombinu mingine ya kuongeza usalama.

Mradi huo pia unatarajiwa kusaidia kupunguza changamoto ya mafuriko katika maeneo kama Mbauda na Kwa Mrombo, ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto za maji wakati wa mvua.

Habari Picha 19016

Kwa sasa, mkandarasi ameanza hatua za awali za kusafisha eneo la mradi huku utekelezaji ukiwa umefikia takribani asilimia tano. Pia zoezi la kuhamasisha mitambo na vifaa vya ujenzi linaendelea

.
TANROADS imesema usanifu wa mradi umekamilika na inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo TANESCO na AUWSA katika kuhamisha miundombinu itakayopisha ujenzi.

Habari Picha 19017

Wananchi Waeleza Matumaini Yao.

Baadhi ya wananchi wa Arusha waliozungumza wakati wa ziara hiyo wameeleza matumaini kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza msongamano wa magari, kuboresha usafiri na kuongeza usalama barabarani..

Habari Picha 19018

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment