Na Bahati Hai .
Kanisa la Evangelical Assemblies of God Tanzania (EAGT-JCC) lililopo Bomang’ombe, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, limefanya huduma ya huruma kwa kutoa vipimo na matibabu kwa wananchi wenye matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo kisukari, presha na matatizo ya macho katika Hospitali ya Wilaya ya Siha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi hilo linalofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Siha, Mchungaji wa kanisa hilo, Sergi Mramba, amesema huduma hiyo inalenga kusaidia wananchi kuboresha afya zao. Zoezi hilo linafanyika kwa siku mbili kuanzia Juni 16 hadi 17, 2026.
“Leo tumekuja hapa kwa ushirikiano na madaktari wa Hospitali ya Wilaya ya Siha kufanya vipimo na matibabu kwa wananchi wenye matatizo ya kisukari, presha pamoja na matatizo ya macho. Lengo letu ni kuona wananchi wanaendelea kuwa na afya njema,” amesema Mramba.Amesema hatua hiyo imekuja baada ya kuonekana kuwa idadi ya watu wanaougua magonjwa yasiyoambukiza imeongezeka kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha, huku gharama za matibabu zikiwa ni changamoto kwa baadhi ya wananchi.
Mramba amesema huduma hiyo inatolewa bure kwa ushirikiano kati ya kanisa hilo na marafiki zao kutoka nchini Marekani, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jamii na kuboresha afya za wananchi.


Ameongeza kuwa huduma kama hiyo imewahi kufanyika katika maeneo mbalimbali na ni mwendelezo wa matendo ya kiimani yanayolenga kuonesha upendo, umoja na mshikamano kwa jamii.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha, Nsubili Mwakapeje, amelipongeza kanisa la EAGT kwa kujitolea kutoa huduma hizo kwa wananchi, akisema wamechagua kusaidia katika kituo hicho licha ya kuwepo kwa maeneo mengine yenye uhitaji.


“Pale mlipotoa Mungu awabariki. Tunaomba siku nyingine mfike tena. Ninyi mnatoa huduma za kiroho na sisi tunatoa huduma za kimwili,” amesema Mwakapeje.
Mwisho.

