SIMANZI YATAWALA MAZISHI YA MJUMBE WA SERIKALI KWARE ALIYEUAWA KIKATILI KWA KUPIGWA MAWE

Geofrey Steven
2 Min Read

HAI, KILIMANJARO .

Vilio na simanzi vimetawala katika mazishi ya Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kware, Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Nickison Usiri (40), ambaye pia alikuwa mfanyabiashara na mfugaji. Marehemu alifariki dunia baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa kupigwa mawe sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwemo kichwani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa mahojiano huku uchunguzi ukiendelea kubaini waliohusika na mauaji hayo.

Habari Picha 18663

Mazishi ya marehemu yamefanyika leo, Juni 6, 2026, katika Kijiji cha Kware, yakihudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa dini, serikali na wananchi kutoka maeneo mbalimbali. Viongozi hao wamelaani tukio hilo wakisema ni la kinyama na lisilokubalika katika jamii.

Akizungumza baada ya mazishi yaliyofanyika katika makaburi ya Kanisa la KKKT karibu na Shule ya Msingi Kware, Afisa Tarafa wa Masama, Nsajigwa Ndagile, ameitaka jamii kumrudia Mungu, kudumisha upendo na amani, pamoja na kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi.

“Matukio kama haya yanapaswa kutufundisha kumtegemea Mungu na kuishi kwa upendo. Tuwe na subira, tumuombee marehemu na tukubali kuwa yote ni mapenzi ya Mungu,” amesema Ndagile.

Habari Picha 18664
Habari Picha 18665

Aidha, amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria.

Kwa upande wake, baba wa marehemu, Elias Usiri, amesema familia bado haijafahamu chanzo cha mauaji hayo. Ameeleza kuwa marehemu ameacha watoto watatu pamoja na mke wake ambaye ni mama wa mtoto mwenye umri wa wiki moja.

Habari Picha 18666

Ameiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo, huku sheria ikichukua mkondo wake.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, Nickison Usiri aliuawa Juni 1, 2026, majira ya mchana akiwa anachunga ng’ombe katika eneo lililo karibu na kijiji hicho. Mwili wake ulikutwa ukiwa umeuawa na kutupwa pembezoni mwa mashamba ya mahindi.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Mwisho…

Share This Article
Leave a Comment