MAONESHO YA KARIBU-KILIFAIR YAZINDULIWA ARUSHA, SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUIMARISHA SEKTA YA UTALII.

Geofrey Steven
2 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha sekta ya utalii nchini kwa kuwekeza zaidi katika miundombinu, kuboresha viwango vya malazi na huduma za ukarimu, pamoja na kuimarisha ubora wa utoaji wa huduma kwa watalii.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair yanayofanyika mkoani Arusha, tukio ambalo limekusanya wadau wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Habari Picha 18597

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bi. Theresa Mugobi, amesema serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza sekta hiyo ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kunufaika na mapato ya fedha za kigeni pamoja na mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Habari Picha 18599
Habari Picha 18598

Bi. Mugobi amesema uwekezaji katika sekta ya utalii utaenda sambamba na juhudi za kuitangaza Tanzania katika masoko ya jadi na yale yanayoibukia duniani, ikiwemo Afrika, Ulaya, Asia, Mashariki ya Kati na Amerika.

“Lengo la serikali ni kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii la kimataifa kwa kuimarisha masoko mapya na kuendeleza yale ya jadi, jambo litakalosaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu pamoja na mapato yatokanayo na sekta hii,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa Karibu-KiliFair, Bw. Dominic Shoo, amesema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa kampuni za utalii, waendeshaji wa safari na wadau wengine wa sekta hiyo kutangaza na kuuza bidhaa za utalii za Tanzania katika soko la kimataifa.

Habari Picha 18600
Habari Picha 18601

Amesema washiriki kutoka zaidi ya nchi 50 wamejitokeza kushiriki maonesho ya mwaka huu, jambo linalodhihirisha kukua kwa umuhimu wa Karibu-KiliFair katika kuunganisha wadau wa utalii duniani.

Bw. Shoo pia ameiomba serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa waandaaji wa maonesho hayo ili kuongeza ufanisi katika juhudi za kuitangaza Tanzania na kuvutia watalii zaidi kutoka masoko mbalimbali duniani.

Habari Picha 18602
Habari Picha 18603

Maonesho ya Karibu-KiliFair yanaendelea kuwa moja ya matukio makubwa ya utalii Afrika Mashariki, yakitoa fursa kwa wadau wa sekta hiyo kujenga ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kutangaza vivutio vya kipekee vinavyopatikana Tanzania.

Habari Picha 18606
Habari Picha 18605

 

Mwisho..

Share This Article
Leave a Comment