Na Mwandishi Wetu
WACHAMBUZI huru Ahmed Kombo na Joseph Yona wamewataka vijana nchini kutokubali kutumika katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha na kuvuruga amani ya taifa, wakisisitiza umuhimu wa kulinda utulivu na mshikamano uliopo nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 31, 2026, wachambuzi hao walisema kuna baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema wanaoendesha mikakati ya kuzichafua taasisi za Serikali kwa maslahi yao binafsi, jambo ambalo linapaswa kukemewa na jamii.

Ahmed Kombo amesema vijana wanapaswa kuwa makini na kuchambua kwa kina taarifa wanazopewa ili kuepuka kushawishiwa kushiriki vitendo vinavyoweza kuleta migawanyiko au kuhatarisha utulivu wa nchi.
Amesema ni muhimu kwa vijana kutambua wajibu wao katika kulinda amani ya taifa na kutokubali kutumiwa na watu wenye malengo ya kuleta taharuki katika jamii kwa maslahi yasiyo na manufaa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Joseph Yona aliziomba mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya watu wanaojaribu kuichafua Tanzania na kuhamasisha uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda usalama na utulivu wa nchi.
Mwisho
