WAUMINI WA KIISLAMU NA WANANCHI HAI WAHIMIZWA KUDUMISHA AMANI NA UPENDO

Geofrey Steven
2 Min Read

Hai, Kilimanjaro

Immamu wa Msikiti wa Shafiy uliopo Bomang’ombe Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Maulid Abdu, amewasihi waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano, huku wakijiepusha na vitendo vinavyochochea vurugu na uvunjifu wa amani.

Wito huo ameutoa Mei 27, 2026, wakati wa hotuba ya Eid El Adha iliyofanyika katika Msikiti wa Shafiy Bomang’ombe na kuhudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Habari Picha 18502

Akizungumza katika hotuba yake, Immamu Maulid amesema kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na mafanikio ya jamii yoyote, huku akieleza kuwa kukosekana kwa amani husababisha mateso makubwa kwa wananchi.
“Tukiangalia baadhi ya nchi duniani zinavyokumbwa na migogoro, tunaona watoto, wazee na kina mama wakiteseka na kukimbia huku na kule wakiwa na mizigo migongoni. Kwa kweli hali hiyo inasikitisha sana,” amesema Maulid.

Aidha, amewaomba Waislamu na Watanzania wote kuendelea kuilinda amani iliyopo nchini kwa kuenzi upendo, mshikamano na kuheshimiana.

Katika hatua nyingine, Immamu huyo amewataka wazazi na walezi kuwalea watoto katika misingi ya dini na maadili mema kwa kufuata mfano wa Mtume Muhammad (S.A.W), ili kujenga jamii yenye kuthaminiana, kupendana na kuishi kwa amani.

Habari Picha 18503
Habari Picha 18504

“Malezi bora yanaanzia nyumbani kwa kuwajenga watoto katika misingi ya dini na maadili mema, jambo litakalosaidia kuwa na jamii imara inayodumisha amani,” ameongeza.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaaban Mlewa, amewahimiza Waislamu kuitumia vyema siku ya Eid El Adha kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kupitia ibada ya kuchinja, pamoja na kuwaonyesha huruma na upendo watu wasiojiweza wakiwemo masikini.

Habari Picha 18505

Amesema lengo la ibada hiyo ni kuimarisha mshikamano katika jamii ili wenye uwezo na wasio na uwezo waweze kusherehekea kwa pamoja kwa furaha na upendo.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment