NaGeofrey Stephen Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Waandishi Waendesha Ofisi katika kuhakikisha viongozi na watendaji wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Kitaaluma wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika katika Ukumbi wa Ngurdoto, mkoani Arusha, Makamu wa Rais alisema Serikali inaendelea kuipa uzito taasisi hiyo kutokana na nafasi yake muhimu katika kuimarisha utulivu, mshikamano na utoaji huduma bora kwa wananchi.

Amesema Waandishi Waendesha Ofisi ni sura ya taasisi wanazozifanyia kazi kwani mara nyingi ndiyo hupokea na kuwahudumia wananchi wanaofika kutafuta huduma mbalimbali. Kutokana na hilo, aliwataka kuendelea kuwa wakarimu, wenye heshima na kutoa huduma kwa weledi mkubwa ili kuwafariji na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.


Aidha, Makamu wa Rais aliwasisitiza watumishi hao kuendelea kujitambua, kutunza siri za ofisi na kuzingatia maadili ya kazi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.
Katika hatua nyingine, amepongeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kuendelea kuimarisha taaluma hiyo hadi kufikia kiwango cha shahada ya uzamili, hatua ambayo imewawezesha Waandishi Waendesha Ofisi kushiriki katika maamuzi ya kisera, upangaji wa mikakati pamoja na utekelezaji wake.

Makamu wa Rais pia alivitaka vyuo vinavyotoa mafunzo hayo kuendelea kujiendeleza ili kuzalisha wataalamu wenye uwezo mkubwa wa kulisaidia Taifa. Sambamba na hilo, alizitaka taasisi mbalimbali nchini kuwawezesha Waandishi Waendesha Ofisi kushiriki mikutano ya kitaaluma kwa ajili ya kuongeza ujuzi na uzoefu.

Pia aliwapongeza viongozi wanaomaliza muda wao wa uongozi ndani ya TAPSEA kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha umoja na maendeleo ya wanachama. Aidha, aliwataka wanachama kufanya uchaguzi wa haki, huru na usio na ubaguzi ili kupata viongozi bora watakaoendeleza mafanikio ya taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na watumishi wa umma pamoja na uongozi wa TAPSEA katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kiutumishi kwa manufaa ya wanachama wake.
Waziri huyo pia alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kuajiri watumishi wapya 45,000 wa kada mbalimbali katika mwaka wa fedha 2026/27 ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mbali na ajira hizo mpya, Serikali imepanga kuwabadilishia muundo watumishi 5,865 pamoja na kuwapandisha madaraja watumishi 234,921 katika kipindi hicho.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali tayari iliidhinisha ajira mpya 42,500, ikapandisha vyeo watumishi 219,042, kuwabadilishia muundo watumishi 6,198 pamoja na kulipa malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 18,083.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAPSEA, Bi. Zuhura Maganga, amesema taasisi hiyo imeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuimarisha taaluma ya uandishi na uendesha ofisi nchini. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuanzishwa kwa shahada ya utawala pamoja na shahada ya uzamili ya sanaa katika mawasiliano na usimamizi wa ofisi zinazotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.


Mkutano huo umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujadili maendeleo ya taaluma hiyo pamoja na namna ya kuimarisha utendaji kazi wa Waandishi Waendesha Ofisi nchini Tanzania.


Mwishoo.
