VIJANA WAHAMASISHWA KUWEKEZA KWENYE HISA KUJENGA UCHUMI IMARA WA BAADAYE

Geofrey Steven
4 Min Read

Geofrey Stephen .Arusha

Jiji la Arusha limekuwa kitovu cha mjadala muhimu kuhusu mustakabali wa vijana na uchumi wa Tanzania, baada ya viongozi wa CRDB Bank Plc kutoa wito kwa vijana kuingia zaidi katika uwekezaji wa soko la hisa ili kujijengea uhuru wa kifedha na maisha bora ya baadaye.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Profesa Neema Mori, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa benki hiyo unaotarajiwa kufanyika Mei 15 na 16 mwaka huu jijini Arusha.

Habari Picha 18285
Habari Picha 18286

Mkutano huo unakuja ukiwa na kaulimbiu isemayo “Vijana na Uwekezaji katika Hisa,” ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwahamasisha vijana kuona uwekezaji kama nyenzo muhimu ya kujenga maisha yao ya kesho kupitia teknolojia ya kidijitali na masoko ya mitaji.

Profesa Mori alisema kuwa vijana wanapaswa kutumia ubunifu wao na fursa zilizopo katika uchumi wa kidijitali kuwekeza katika hisa, hatua ambayo inaweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kuwa sehemu ya wamiliki wa taasisi kubwa za kifedha nchini.

Habari Picha 18287

“Ni wakati wa vijana kununua hisa na kuwa wawekezaji ili waweze kutumia ubunifu wa kidijitali kuonyesha vipaji vyao na kujikwamua kiuchumi,” alisema Profesa Mori.

Katika mkutano huo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Musa Omari. Aidha, wanahisa watajadili agenda 12 muhimu zikiwemo ripoti ya ukaguzi, uteuzi wa wajumbe wa bodi pamoja na ripoti ya mwaka ya benki hiyo.

Habari Picha 18288

Katika hatua inayodhihirisha ukuaji wa benki hiyo, CRDB imependekeza gawio la shilingi 90 kwa kila hisa mwaka huu, likiongezeka kutoka shilingi 65 zilizotolewa hapo awali. Profesa Mori alisema ongezeko hilo ni ishara ya mafanikio makubwa ya benki pamoja na imani kubwa kutoka kwa wanahisa wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Plc, Dk. Abdulmajid Nsekela, aliwashukuru wanahisa, wateja na bodi ya wakurugenzi kwa mchango wao mkubwa katika mafanikio ya benki hiyo.

Alisema ushirikiano uliopo umeiwezesha CRDB kuendelea kuwa taasisi imara si tu nchini Tanzania bali pia katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia falsafa ya diplomasia ya uchumi.

 

Habari Picha 18290

“CRDB ni zaidi ya benki. Imevuka mipaka ya Tanzania na Afrika Mashariki kupitia falsafa ya diplomasia ya uchumi, jambo lililoifanya kuendelea kuwa imara kwa zaidi ya miaka 30,” alisema Dk. Nsekela.

Aidha, alisema benki hiyo inaingia katika mkutano mkuu wa mwaka huu ikiwa kinara wa utendaji, baada ya kurekodi faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 206 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026.

Kwa mujibu wa Dk. Nsekela, mafanikio hayo yametokana na imani kubwa ya wanahisa na wawekezaji pamoja na mikakati ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu inayotekelezwa na benki hiyo.

Habari Picha 18291

Alisisitiza kuwa dhamira ya CRDB ni kuhakikisha vijana wa leo hawaishii kuwa wateja wa benki pekee, bali wanakuwa wawekezaji wakubwa na sehemu ya nguvu ya uchumi wa taifa katika miaka ijayo.

Kaulimbiu ya mwaka huu, “Vijana na Uwekezaji katika Hisa,” inalenga kuibua kizazi chenye maono ya uwekezaji, matumizi sahihi ya teknolojia na ubunifu wa kidijitali ili kujenga uchumi imara wa baadaye.

 

Habari Picha 18296

 

Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat, akizungumzia mkutano huo wa wanahisa amesema wanajivunia mkutano huo kufanyika jijini Arusha, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kuthamini mchango mkubwa wa wateja wa kanda hiyo.

Amesema CRDB Bank Kanda ya Kaskazini imeendelea kutoa huduma bora, za kisasa na kidijitali zinazokidhi mahitaji ya wateja wa sasa, huku asilimia kubwa ya huduma hizo zikisimamiwa na vijana wenye uelewa mkubwa wa teknolojia na ubunifu wa kisasa.

Aidha, amesema kuletwa kwa mkutano huo Arusha kunadhihirisha nafasi ya jiji hilo kama kitovu muhimu cha huduma za kisasa za kifedha zinazotolewa na CRDB Bank.

 

Habari Picha 18293
Habari Picha 18292

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment