WANAWAKE SIHA WATAKIWA KUEPUKA KWENDA MASHAMBANI PEKE YAO.

Geofrey Steven
2 Min Read

Na Mwandishi wetu Siha .

Wanawake wakulima katika Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, wamehadharishwa kuepuka kwenda mashambani wakiwa peke yao, hasa katika kipindi hiki cha masika, kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu.

Tahadhari hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, kufuatia tukio la mwanamke mmoja kuvamiwa na watu wasiojulikana alipokuwa shambani na kuporwa mbolea aliyokuwa akitumia, pamoja na simu na kitambulisho cha benki. Tukio hilo lilitokea katika mashamba ya Forest, Kata ya Nasai wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu Mei 2, 2026, Timbuka alisema ni muhimu kwa wananchi, hususan wanawake, kuongozana wanapoenda mashambani ili kupunguza hatari ya kushambuliwa na wahalifu.

Habari Picha 17816
Habari Picha 17815

“Ni muhimu kuwa pamoja; mtu asiende shambani peke yake katika kipindi hiki cha masika. Wahalifu wanatumia fursa ya kujificha kwenye mashamba ya mahindi na kuwapora watu mali zao,” alisema.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amemtaka mwanamke aliyeathirika kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Sanya Juu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa. Pia aliwataka viongozi wa vijiji kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuchukua tahadhari.

Habari Picha 17817

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mowo Njamu, Jackison Salewa, alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa mwanamke aliyeporwa ni mkazi wa kijiji hicho. Aliongeza kuwa kipindi cha masika si salama kwa wanawake kwenda mashambani peke yao, hivyo akawahimiza kwenda kwa makundi kwa ajili ya usalama wao.

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment