Na Bertha Ismail
Arusha. Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk Nicas Mawazo, amejitosa katika kinyang’anyiro cha uongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho, Aprili 22, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Mawazo anawania nafasi ya uenyekiti wa ALAT, nafasi inayoshikiliwa kwa sasa na Murshid Hashim Ngese, na anatarajiwa kuchuana na wagombea wengine akiwemo Sima Constantine Sima wa Mwanza pamoja na Maximilian Iranghe wa Arusha jiji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 21, 2026, mara baada ya kurejesha fomu ya kuomba ridhaa, Dk Mawazo amesema ana lengo la kuleta mageuzi makubwa yatakayoiimarisha ALAT katika kusimamia maendeleo ya serikali za mitaa nchini.
Amesema uamuzi wake umetokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika uongozi pamoja na uelewa wa changamoto zinazokabili halmashauri mbalimbali nchini.

“Nimekuja kurejesha fomu ya uchaguzi wa ALAT ili kuomba ridhaa ya kuongoza taasisi hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu”
” Nikichaguliwa, nitahakikisha ALAT inaimarishwa zaidi ili iwe chombo madhubuti cha kuwasemea wananchi na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali,” amesema.
Ameongeza kuwa ALAT ina nafasi kubwa ya kuisaidia serikali kufikisha huduma kwa wananchi, ikiwemo elimu, afya, barabara na huduma nyingine muhimu za kijamii.
“Sisi ndio tunaoletewa fedha na kuzielekeza kwenye miradi ya wananchi kama hospitali, shule, barabara na huduma nyingine muhimu,” .
Dk Mawazo amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa na ALAT, bado kuna haja ya kuimarisha mifumo yake ya uendeshaji ili kuongeza ufanisi na matokeo chanya kwa jamii.
“ALAT ina mafanikio, lakini nikipata nafasi nitaleta mabadiliko makubwa kutokana na uzoefu wangu wa uongozi. Ninaamini naweza kuongoza taasisi hii kwa ufanisi zaidi,”.
Mkutano huo wa uchaguzi unatarajiwa kufanyika kesho Aprili 22, 2026, ambapo utafunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Lameck Nchemba.
Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT, Thomas Vungwa, amesema mkutano huo wa siku mbili utahusisha uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Amesema wajumbe kutoka halmashauri 184 nchini wanatarajiwa kushiriki.
Amesema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu ulianza Aprili 17, 2026 na unatarajiwa kufikia hitimisho kesho sambamba na kuanza kwa uchaguzi huo.
Mwisho

