Serikali ya Tanzania imechukua hatua mpya katika kuimarisha sekta ya nishati baada ya kukabidhi vitendea kazi vya kisasa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Arusha. Hatua hii inalenga kuongeza kasi ya utoaji huduma, kupunguza hitilafu za umeme na kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi, hasa katika maeneo ya pembezoni.
Hafla ya makabidhiano hayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa sekta ya nishati, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alisisitiza umuhimu wa kulinda na kutumia ipasavyo rasilimali hizo za umma.
Alieleza kuwa serikali imetumia takribani shilingi bilioni 1.4 kununua magari hayo, yakiwemo yenye kreni, magari ya kiutendaji pamoja na bajaji. Lengo kuu ni kuboresha huduma za umeme mijini na vijijini, na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati.
Mkude alitoa onyo kali kwa watumishi wa TANESCO dhidi ya matumizi mabaya ya magari hayo, akisisitiza kuwa ni mali ya walipa kodi na yanapaswa kutumika kwa uadilifu mkubwa.
“Hatutavumilia matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali hizi kwa maslahi binafsi. Lazima zitumike kwa manufaa ya wananchi wote,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Mhandisi Kisika Kisika, alisema ujio wa vitendea kazi hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa serikali ya awamu ya sita chini ya Samia Suluhu Hassan, unaolenga kuzipa taasisi za umma uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Alifafanua kuwa Mkoa wa Arusha una hali nzuri ya upatikanaji wa umeme, ukipokea nishati kutoka vituo vikuu vya Njiro, Lemguru na Karatu. Hali hii inaweka mazingira mazuri kwa uwekezaji, hasa katika sekta za viwanda na biashara. Hata hivyo, alibainisha changamoto ya matumizi duni ya umeme, akisema kuwa mkoa unatumia takribani asilimia 30 tu ya umeme unaozalishwa, huku zaidi ya asilimia 60 ikiwa bado ni ziada.
“Hii ni fursa kubwa kwa wawekezaji kuja kuwekeza Arusha, kwani nishati ya uhakika ipo ya kutosha,” alisema.Kwa sasa, TANESCO Arusha ina zaidi ya wateja laki tatu, idadi inayoongezeka kila mwaka kutokana na jitihada za serikali kusambaza umeme hadi vijijini. Karibu vijiji vyote tayari vimefikiwa na huduma hiyo, huku hatua zikichukuliwa kuhakikisha vitongoji vyote vinaunganishwa.
Ujio wa magari haya mapya unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma, kwa kuwezesha mafundi kufika haraka kwenye maeneo yenye hitilafu na kuboresha mawasiliano na wateja.
Serikali imeendelea kusisitiza kuwa itaendelea kuwekeza katika sekta ya nishati ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, uongozi wa TANESCO Mkoa wa Arusha umeahidi kuyatunza na kuyatumia ipasavyo vitendea kazi hivyo, ili kuhakikisha vinatoa matokeo chanya kwa jamii na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Mwisho.
Sign Up For Daily Newsletter
Be keep up! Get the latest breaking news delivered straight to your inbox.
[mc4wp_form]
By signing up, you agree to our Terms of Use and acknowledge the data practices in our Privacy Policy. You may unsubscribe at any time.