SERIKALI YATAKIWA KUELEZA HATMA YA UJENZI WA SOKO LA KISASA NGARAMTONI,

Geofrey Steven
2 Min Read

Na Mwadishi A24tv .Dodoma .

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Johannes Lukumay, ameibua hoja nzito bungeni akiitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu lini itaanza ujenzi wa soko la kisasa katika eneo la Ngaramtoni—ahadi iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake mkoani Arusha.

Akiwasilisha swali lake bungeni, Lukumay alieleza kuwa wananchi wa Arumeru Magharibi wameendelea kuwa na matarajio makubwa ya kunufaika na mradi huo, ambao unaonekana kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya biashara na kuinua uchumi wa eneo hilo.

Alikumbusha kuwa tarehe 1 Oktoba 2025, Rais alifanya ziara katika jimbo hilo na kuahidi ujenzi wa soko la kisasa Ngaramtoni. Hata hivyo, hadi sasa hakuna dalili za utekelezaji wa ahadi hiyo, jambo linalozua maswali na wasiwasi miongoni mwa wananchi.

Habari Picha 16996

“Wananchi wa Ngaramtoni na maeneo jirani bado wanafanya biashara katika mazingira yasiyoridhisha. Ni muhimu Serikali ikaeleza ni lini hasa ujenzi wa soko hilo utaanza,” alisisitiza Lukumay.

Mbunge huyo alifafanua kuwa ujenzi wa soko hilo utakuwa chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Arumeru Magharibi, hasa ikizingatiwa kuwa Ngaramtoni ni kitovu muhimu cha shughuli za biashara na kilimo. Aliongeza kuwa soko la kisasa litasaidia kuongeza mapato ya halmashauri, kuboresha usafi na usalama wa wafanyabiashara, pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta ndogo na za kati.

Hoja hiyo imeibuliwa wakati Serikali ikiendelea kusisitiza dhamira yake ya kuboresha miundombinu ya masoko nchini ili kuwawezesha wananchi kufanya biashara katika mazingira bora na yenye tija.

Kwa sasa, macho ya wananchi wa Arumeru Magharibi yanaelekezwa serikalini wakisubiri majibu ya kina pamoja na hatua madhubuti za utekelezaji wa ahadi hiyo muhimu kwa maendeleo yao.

Share This Article
Leave a Comment