Geofrey Stephen Karatu .
MKUU wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, ameweka bayana hali ya bwawa la Bwawani lililopo Karatu Mkoani Arusha kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha,
akisisitiza kuwa serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa maji pamoja na usalama wa wananchi kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama ya Wilaya na Kamati za Maafa.
Akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa maeneo mbalimbali, Karanga alisema kuwa bwawa hilo hujaa maji katika msimu wa mvua kama ilivyo kawaida, huku akibainisha kuwa hatua za kitaalamu zimekuwa zikichukuliwa ili kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza.

Alitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni pamoja na uwekaji wa miundombinu ya kudhibiti maji, ikiwemo pampu za kuvuta maji pamoja na uboreshaji wa mifereji ya kupitisha maji ya mvua ili kuzuia maji kutwama katika bwawa hilo.

“Ni kweli kabisa Karatu tunalo bwawa ambalo hujaa maji kipindi hiki cha mvua, lakini tupo makini kulifuatilia ili kuhakikisha halileti athari kwa wananchi wanaoishi jirani nalo,” alisisitiza.
Aidha, alieleza kuwa serikali ya wilaya imeimarisha ushirikiano na kamati za maafa, viongozi wa mitaa na madiwani katika kufanya tathmini za mara kwa mara, hatua inayolenga kudhibiti madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.
Katika hatua nyingine, Karanga amesema hadi sasa yupo uwanjani akiongoza juhudi za pamoja na wananchi katika kurekebisha miundombinu iliyoathirika, ikiwemo barabara, mitaro na njia za maji, ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi zinaendelea bila vikwazo vikubwa.
Amesema kasi ya maboresho hayo inaendelea kuongezwa ili kurejesha hali ya kawaida haraka iwezekanavyo, huku akisisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua zaidi pale inapobidi.
Wakati huo huo, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuepuka makazi katika maeneo hatarishi, hususan yale yaliyo karibu na mikondo ya maji.
“Ni muhimu kwa wananchi kuacha kupuuza mvua hizi. Tunapaswa kuchukua hatua za kujilinda mapema, ikiwemo kuhama maeneo yenye hatari ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika,” alisisitiza.
Alionya kuwa uzembe katika kuchukua tahadhari unaweza kusababisha upotevu wa nguvu kazi ya taifa, jambo ambalo linaathiri moja kwa moja maendeleo ya jamii na uchumi wa eneo hilo.
Akizungumzia sekta ya utalii, Karanga alisisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya barabara ni muhimu katika kuimarisha shughuli za utalii, akibainisha kuwa Wilaya ya Karatu ni lango kuu la kuelekea Hifadhi ya Ngorongoro.

Alisema kuwa wanahakikisha barabara zinapitika wakati wote ni hatua muhimu ya kukuza utalii na kuchochea uchumi wa eneo hilo pamoja na taifa kwa ujumla.
Karanga amehitimisha kwa kusisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mkazo katika ufuatiliaji wa miundombinu ya maji pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi, ili kuhakikisha usalama wa maisha na mali unaimarishwa katika kipindi hiki cha mvua kubwa.
Mwisho .

