BAKWATA KILIMANJARO YASHANGAZWA DAWA ZA KULEVYA KUUZWA WAZIWAZI, YATAKA VIONGOZI WA MITAA WACHUKUE HATUA

a24tv
2 Min Read

Na bahati Moshi.

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Kilimanjaro limesema linasikitishwa na kuendelea kuuzwa kwa dawa za kulevya kwa uwazi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo bangi na mirungi, huku baadhi ya viongozi wa ngazi za chini wakionekana kutokuchukua hatua stahiki.
Akizungumza Machi 16, 2026, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa, katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu, nyumbani kwake Moshi, alisema hali hiyo inachangia kuangamia kwa vijana na kuhatarisha mustakabali wa taifa.

Sheikh Mlewa alisema matumizi ya mihadarati yameongezeka miongoni mwa vijana, akitaja unywaji wa pombe, ulaji wa mirungi na uvutaji wa bangi kuwa sasa vinafanyika hata katika maeneo ya wazi bila hofu yoyote. Alieleza kushangazwa na hali hiyo kuendelea wakati viongozi wa vitongoji, vijiji, kata, watendaji na madiwani wakiwa kwenye maeneo yao.

Habari Picha 11466

Alionya kuwa viongozi wanaokaa kimya bila kuchukua hatua dhidi ya wauza na watumiaji wa dawa hizo wanaweza kutafsiriwa kama washirika wa uharibifu unaoendelea kwa vijana. Alisisitiza kuwa si lazima Mkuu wa Mkoa ashuke hadi ngazi za chini kupambana na tatizo hilo wakati wapo viongozi wenye mamlaka katika maeneo husika wanaoweza kulisimamia.

Kwa upande mwingine, Sheikh Mlewa alisema viongozi wa dini wanaendelea kuwajenga vijana katika maadili mema, lakini juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono na serikali pamoja na taasisi nyingine kwa kuwakamata wahusika na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuandaa hafla hiyo ya futari iliyowakutanisha watu wa makundi mbalimbali, akisema ni hatua inayodhihirisha umoja wa Watanzania.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema atalifanyia kazi suala hilo kadiri ya uwezo wake ili kusaidia kukabiliana na tatizo la matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana.

Habari Picha 11467

Aidha, aliwashukuru wote waliohudhuria futari hiyo nyumbani kwake na kueleza kufurahishwa na mwitikio wao.

Share This Article
Leave a Comment