Na Bahati Kilimanjaro .
Wanafunzi wa kidato cha sita kutoka Shule ya Sekondari Modio Islamic Seminar wilayani Hai, mkoa wa Kilimanjaro, wametembelea kitengo cha Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC na kutoa sadaka ya vitu mbalimbali kwa wagonjwa.
Miongoni mwa vitu walivyotoa ni unga wa ulezi, sabuni za kufulia na biskuti, ikiwa ni sehemu ya matendo ya huruma na kusaidia wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika kitengo hicho.

Wanafunzi hao wamesema lengo la kutoa sadaka hiyo ni kutimiza mafundisho ya dini ya kuwatembelea wagonjwa, kuwafariji pamoja na kufanya amali njema, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu awape wepesi na mafanikio katika mitihani yao inayotarajiwa kufanyika mwezi Mei 2026.
“Ukitaka jambo lako lifanikiwe ni vizuri kutanguliza unyenyekevu na kufanya amali njema. Sisi tumekuja kuwatembelea wagonjwa, kuwajulia hali na kutoa kile kidogo tulichobarikiwa na Mungu,” walisema wanafunzi hao.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Aimani Muhamed, alisema ziara hiyo imelenga pia kuwatembelea watoto wenye saratani na kuwafariji kwa kuwapatia msaada mdogo waliobarikiwa nao.

Kwa upande wake, Lightness Swai, mzazi anayemuuguza mtoto wake katika hospitali hiyo, aliwashukuru wanafunzi hao kwa moyo wa kujitolea na kujali wagonjwa.
“Nawashukuru sana kwa upendo wenu na sadaka mlizotuletea. Mungu awabariki na muendelee kuwa na moyo huo hata mtakaporudi kwenye jamii baada ya kumaliza mitihani yenu,” alisema.
Naye Robert Kessy, mratibu msaidizi wa wauguzi katika kitengo cha Saratani KCMC, alisema kitendo hicho ni cha kupongezwa kwani kinawafariji wagonjwa pamoja na wazazi wao.

Mkuu wa shule hiyo, Athumani Mtavangu, alisema mafunzo wanayoyatoa shuleni hapo hayaishii darasani pekee bali pia yanasisitiza wanafunzi kuishi kwa vitendo katika jamii.
Alisema ziara hiyo imelenga kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa kufanya matendo mema na kuwasaidia wahitaji ili wanaporudi katika jamii waendelee kuwa na moyo wa kujali wengine.

Mwisho.

