
Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) ni chama cha kitaaluma cha wauguzi nchini kilichoanzishwa kisheria chini ya Sheria ya Vyama vya Kijamii na Kitaaluma (Societies Ordinance Act), 1954 (Rule 5). Moja ya malengo makuu ya chama ni kuimarisha ubora wa huduma za kiuguzi kwa kuhamasisha sera bora zinazolenga kuboresha huduma za afya, kutetea haki na wajibu wa wauguzi katika utoaji wa huduma bora, pamoja na kuhakikisha wanataaluma wanatoa huduma kwa kuzingatia weledi, maadili ya taaluma na miongozo iliyowekwa.
Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kimepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa zilizoanza kusambaa kuanzia tarehe 04 Machi 2026 kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii. Taarifa hizo zinahusu kauli iliyotolewa na Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wa Tanzania, kuhusu tukio la mtu anayedaiwa kuwa muuguzi aliyemchukua mgonjwa na kumfanyia upasuaji nyumbani kwake juu ya makochi.
Tendo hilo linalodaiwa kufanywa ni kinyume kabisa na Maadili ya Taaluma ya Uuguzi (Professional Code of Conduct), viapo vya kitaaluma, pamoja na sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma nchini.
Ufuatiliaji na Ubainifu.
Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, uongozi wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Taifa ulifanya ufuatiliaji wa haraka katika mkoa husika. Baada ya uchunguzi wa awali, chama kinapenda kuubainishia umma yafuatayo:
1. Utambulisho wa Mhusika
Imebainika kuwa mhusika anayedaiwa kufanya kitendo hicho siyo muuguzi na hana sifa wala taaluma ya uuguzi. Badala yake, mhusika ni mtumishi wa idara ya afya katika Wilaya ya Urambo, Mkoa wa Tabora, anayefanya kazi katika Zahanati ya Kamsekwa Dispensary akiwa katika nafasi ya Mhudumu wa Afya (Health Attendant).
2. Kutohusika kwa Taaluma ya Uuguzi
Kwa kuzingatia utambulisho huo, tuhuma hizi hazihusiani na muuguzi yeyote na haziakisi utendaji wa taaluma ya uuguzi nchini.
3. Hatua za Kisheria.
Chama cha Wauguzi Tanzania kinaziomba na kuzihimiza mamlaka zinazomsimamia mhusika husika (mwajiri pamoja na vyombo vya kisheria) kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na miongozo ya nchi ili kukomesha vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.
4. Wito kwa Mamlaka na Wadau.
Chama kinatoa wito kwa mamlaka zinazohusika na utoaji wa taarifa kwa umma kuhakikisha zinajiridhisha kikamilifu kuhusu utambulisho na taaluma za watuhumiwa kabla ya kutoa taarifa rasmi. Hatua hii itasaidia kuepuka kudhalilisha taaluma na wanataaluma wasiohusika, pamoja na kuzuia taharuki na sintofahamu ndani ya sekta ya afya.
Aidha, chama kinawasihi wauguzi wote nchini kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma katika utoaji wa huduma. Ni wajibu wa kila muuguzi kuhakikisha huduma bora, salama na zenye viwango vya juu zinatolewa katika maeneo rasmi ya kutolea huduma za afya pekee.
5. Hitimisho
Mwisho, Chama cha Wauguzi Tanzania kinawapongeza wauguzi wote nchini kwa kazi yao kubwa na ya kujitolea katika kulinda na kuimarisha afya za Watanzania. Chama kitaendelea kulinda hadhi na heshima ya taaluma ya uuguzi na kuhakikisha huduma zinazotolewa na wanataaluma zinazingatia viwango na miongozo iliyowekwa.
Imetolewa na:
Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA)

