Geofrey Stephen Arusha –
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imesaini hati ya makubaliano (MOU) na taasisi binafsi ya Global Education Link Ltd kwa lengo la kushirikiana katika nyanja za kitaaluma, uwekezaji na teknolojia.
Makubaliano hayo yamesainiwa Jumanne, Machi 10, 2026 katika makao makuu ya taasisi hiyo jijini Arusha. Hati hizo zilisainiwa na Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Global Education Link Ltd, Abdulmalik Mollel.

Alieleza kuwa NM-AIST ilianzishwa kwa dhamira ya kuzalisha kizazi cha wanasayansi na wabunifu mahiri waliobobea katika sayansi, teknolojia na ubunifu. Lengo kuu ni kuwaandaa vijana watakaoweza kuleta mageuzi na mapinduzi ya kiuchumi katika jamii ya Tanzania.


Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Global Education Link Ltd, Abdulmalik Mollel, alisema taasisi yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa ili kuongeza tija katika elimu na uwekezaji.
Mollel alisema uzoefu wake unaonyesha kuwa vyuo vikuu katika mataifa yaliyoendelea vinaunganisha elimu, uwekezaji na teknolojia kwa namna inayochochea maendeleo ya kiuchumi ya nchi zao.

“Tunashuhudia jinsi elimu inavyotumika kama chombo cha kutatua changamoto za kiuchumi kupitia maarifa wanayopata vijana katika vyuo vikuu,” alisema.
Aliongeza kuwa mataifa yaliyoendelea yamefanikiwa kwa sababu yaliwekeza katika vituo vya tafiti na teknolojia, jambo lililosaidia kubadilisha uchumi wa nchi zao.


“Kwa hakika, hakuna mabadiliko ya kweli ya kiuchumi yanayoweza kupatikana bila uwekezaji katika tafiti kutoka taasisi za elimu ya juu,” alisisitiza.


Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa mpya za elimu, tafiti na uwekezaji, huku ukiimarisha nafasi ya NM-AIST kama kituo muhimu cha maendeleo ya sayansi na teknolojia barani Afrika.


Mwishooo..

