Siha, Kilimanjaro.
Wananchi wa Kijiji cha Donyomurwak, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuharakisha usajili wa Shule Mpya ya Sekondari ya Mondo Memusi ili ianze kufanya kazi kikamilifu na kuwanufaisha watoto wa jamii hiyo, hususan jamii ya wafugaji.
Ombi hilo limetolewa leo Januari 17, 2026, katika hafla fupi iliyofanyika katika Kijiji cha Oloiwang, wakati Shirika la Mondo UK kwa kushirikiana na Mondo Tanzania lilipokabidhi rasmi shule hiyo kwa Serikali baada ya ujenzi wake kukamilika.
Changamoto ya Umbali Mrefu Kwa Wanafunzi.

Wananchi wamesema ujenzi wa shule hiyo umekuja kuondoa changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wanafunzi waliokuwa wakitembea kilometa 24 kila siku (kwenda na kurudi) kusoma katika Shule ya Sekondari Sekirari.
“Kwa muda mrefu watoto wetu walikuwa wakiamka saa kumi usiku kuanza safari ya kwenda shule. Walifika wakiwa wamechoka, wengine wakichelewa masomo na wasichana wakikumbana na hatari ya kupata ujauzito kutokana na umbali mrefu,” amesema Paulina Israel, mkazi wa eneo hilo.

Amesema kutokana na changamoto hizo, wananchi na viongozi waliamua kuanzisha ujenzi wa shule hiyo hadi hatua ya msingi kabla ya Shirika la Mondo UK na Mondo Tanzania kuunga mkono jitihada hizo.
Mchango wa Mondo UK na Mondo Tanzania
Kupitia ushirikiano huo, shule imefanikiwa kujengwa kwa:
Vyumba vya madarasa 4
Ofisi za walimu 2
Matundu ya vyoo 12 kwa wanafunzi
Meza 100 na viti 100.
Paulina amesema kukamilika kwa ujenzi huo kumeleta matumaini makubwa kwa wananchi, huku wakisisitiza kuwa kilichobaki ni usajili wa shule ili wanafunzi waanze masomo mara moja.


Serikali Yatoa Ahadi ya Usajili wa Haraka.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema Serikali itaharakisha usajili wa shule hiyo ndani ya mwezi Januari 2026.
“Hatuwezi kuacha shule hii ikae muda mrefu bila kusajiliwa wakati lengo lake ni kupunguza umbali kwa watoto waliokuwa wakitembea kilometa 24 kila siku. Ndani ya mwezi huu shule itasajiliwa na wanafunzi watahamishwa kutoka Sekirari,” amesema Timbuka.
Amepongeza jitihada za wadau wa maendeleo akiwemo Mwalimu Meijo Laizer kwa mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu wilayani humo.


CCM Yasifu Mchango wa Wadau wa Maendeleoisia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha, Alfred Mosi, amesema ujenzi wa shule hiyo ni mfano mzuri wa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu.
Amepongeza Shirika la Mondo UK na Mondo Tanzania kwa kujitolea kujenga na kukabidhi miradi ya elimu kwa Serikali, akisema ni jambo la kuigwa na wadau wengine.
Miradi Mengine ya Elimu Oloiwang.
Awali, katika taarifa yake, Mwalimu Meijo Laizer, mdau wa maendeleo wilayani humo, amesema katika Kijiji cha Oloiwang, Shirika la Mondo UK kwa kushirikiana na Mondo Tanzania limejenga:
Vyumba vya madarasa 2
Matundu ya vyoo 12
Madawati 50.
Ameongeza kuwa jumla ya gharama za miradi ya elimu katika vijiji vya Donyomurwak na Oloiwang ni zaidi ya shilingi milioni 200, akilishukuru shirika hilo kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya watoto wa jamii za pembezoni.
Hitimisho.
Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mondo Memusi ni ushahidi wa nguvu ya ushirikiano kati ya wananchi, viongozi na wadau wa maendeleo. Wananchi sasa wana matumaini mapya kuwa ndoto ya watoto wao kusoma karibu na makazi yao .
Mwisho .



