Na Geofrey Stephen Arusha .Wizara ya Fedha imewataka wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hatua inayolenga kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Wito huo umetolewa leo, Desemba 19, 2025, na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, kwa niaba ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Munde, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 16 wa Mwaka wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, unaosimamiwa na Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) na kufanyika jijini Arusha.
Mchango wa Ununuzi na Ugavi katika Maendeleo ya Taifa.


Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Omar alisema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa wataalamu wenye sifa stahiki, maadili ya juu na wanaozingatia sheria, kanuni na mifumo iliyowekwa.
Alieleza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ununuzi na ugavi kwa kuunganisha mfumo wa usajili wa wataalamu wa PSPTB na Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki (NeST), hatua inayolenga kuhakikisha uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
“Hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana bila mifumo madhubuti ya ununuzi na ugavi. Serikali inaendelea kusisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuzuia mianya ya ubadhirifu,” alisema Balozi Omar.
Onyo kwa Wanaokiuka Sheria
Waziri huyo alitoa onyo kali kwa watu wanaotekeleza shughuli za ununuzi na ugavi bila kuwa na sifa stahiki, hususan katika mamlaka za serikali za mitaa, akisisitiza kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi na Ugavi na hakitavumiliwa.


Aidha, aliihimiza sekta binafsi kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu za ununuzi na ugavi, akibainisha kuwa sekta hiyo ni mdau muhimu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Taifa.
Mafanikio ya PSPTB.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PSPTB, Jacob Kibona, alisema bodi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo kusimamia na kuendeleza mitaala ya kitaaluma inayolenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, maarifa na maadili ya taaluma ya ununuzi na ugavi.

Aliongeza kuwa PSPTB imeendelea kutoa mafunzo endelevu ya maendeleo ya kitaaluma (CPD) kwa wataalamu pamoja na kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali, hususan mfumo wa usajili, hatua inayoongeza uwazi na ufanisi katika sekta hiyo.
Mwisho .



