Na Geofrey Stephen Arusha .
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, ameliagiza Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuimarisha usimamizi wa mapato, kusimamia miradi ya maendeleo na kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa kwa wakati, akisisitiza kuwa mapato ni msingi wa maendeleo ya Halmashauri yoyote.
Mapato ni Msingi wa Huduma Bora
Akizungumza leo Jumanne, Disemba 16, 2025, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha, Mhe. Makalla amesema kuwa bila ukusanyaji mzuri wa mapato, Halmashauri haiwezi kutoa huduma bora kwa wananchi.



“Mapato ni msingi wa Halmashauri katika kuwahudumia wananchi. Wekeni mikakati ya kukusanya na kusimamia vyanzo vya mapato, pamoja na kuboresha huduma katika maeneo ya mapato ikiwemo masoko. Takwimu za ukusanyaji bado haziridhishi,” amesema Mhe. Makalla.
Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo
Mhe. Makalla amewataka madiwani kuwa mstari wa mbele katika kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mikataba.
Miradi hiyo ni pamoja na:
- Kituo Kikuu cha Mabasi
- Soko la Kilombero
- Uwanja wa Michezo Bondeni City
- Jengo la Utawala la Halmashauri ya Jiji la Arusha
Amesisitiza kuwa miradi hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa jiji na kuboresha maisha ya wananchi.


Barabara, Usafi na Hadhi ya Jiji la Kitalii
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa ameitaka TARURA kushirikiana kwa karibu na madiwani katika kutatua kero za barabara kwenye mitaa mbalimbali. Pia amesisitiza suala la usafi wa mazingira ili Jiji la Arusha liendane na hadhi yake kama jiji la kitalii.
Aidha, amehimiza ukuzaji wa utalii wa michezo kama fursa mpya ya kiuchumi kwa vijana na wananchi wa jiji hilo.
Uwazi Katika Mikopo ya Asilimia Kumi
Mhe. Makalla amesisitiza uwazi na haki katika utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, akiwataka madiwani kuhakikisha mikopo hiyo inawafikia walengwa waliokusudiwa bila.


upendeleo.
Madiwani Kuwa Karibu na Wananchi
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Makalla amewataka madiwani kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa vitendo.
“Wananchi wanahitaji viongozi wanaosikiliza na kuchukua hatua. Hapo ndipo imani ya wananchi kwa Serikali yao inapojengwa,” amesisitiza.
Mwisho .



