Na Mwandishi Wetu
MBEYA: Daktari wa Mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dkt. Angela Mlingi, amesema wamewahudumia jumla ya wagonjwa 472, wengi wao wakiwa na matatizo ya afya yanayohusiana na mgongo na nyonga.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayomalizika Oktoba 14, 2025, Dkt. Angela alisema kati ya wagonjwa hao, takribani 40 wamependekezwa kwenda MOI jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi na matibabu ya kina kutokana na hali zao kuhitaji utaalamu maalum.

Ameongeza kuwa wagonjwa wenye hali za wastani wameelekezwa kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, ambayo sasa ina uwezo mkubwa wa kutoa huduma za tiba ya mifupa baada ya madaktari wake kupatiwa mafunzo maalum na wataalamu wa MOI.
“Tunawashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha mwamko wa kutafuta huduma. Hii inaonesha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu kuhusu afya ya mifupa, kwani watu wengi hupuuza dalili za awali kutokana na kutoelewa madhara yake,” alisema Dkt. Angela.
Aidha, amewashauri wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara na kutembelea hospitali mapema wanapohisi mabadiliko yoyote ya kiafya badala ya kusubiri hali kuwa mbaya.
“Wengi wanajua wana matatizo lakini kuchelewa kufika hospitalini kunasababisha hali zao kuwa mbaya zaidi. Tunawahimiza watu wapime afya zao mapema ili matatizo yatibiwe kwa wakati,” alisisitiza.