Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia ustawi wa taifa kwa ujumla.

Mikakati hiyo inahusisha uanzishaji wa mifumo ya kitaasisi, kisera, mipango kazi, miongozo na sheria zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Mary Maganga, wakati akifungua Kongamano la Vijana Tanzania lenye muda wa siku mbili, linalofanyika kuanzia leo 12 Oktoba hadi 13 Oktoba 2025, jijini Mbeya katika Ukumbi wa City Park Garden.
Bi. Maganga alisema lengo la kongamano hilo ni kuwajengea vijana ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, kukuza ushirikiano, kubadilishana mawazo, pamoja na kutambua na kuunga mkono miradi ya vijana inayolenga kuinua uchumi wao.
“Vijana ni nguvu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii zetu. Ni lazima tutumie vyema nguvu hii kubadilisha dunia kuwa mahali bora kwa ajili ya wote,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Aidha, aliwahimiza vijana kutumia kongamano hilo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazowakabili, ili Serikali iweze kuchukua maoni yao na kuyatumia kuboresha sera, sheria, kanuni na miongozo kwa manufaa ya vijana wote nchini.
Sambamba na hilo, Bi. Mary aliwataka vijana kote nchini kujitokeza kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, kwa kuchagua viongozi wanaoakisi matumaini, malengo na ndoto za taifa.

Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogolo, aliwahimiza vijana kuipenda nchi na kujivunia Tanzania, akisisitiza kuwa kila kijana ana mchango muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Seleman Mvunye, alisema kongamano hilo linajumuisha zaidi ya vijana 1,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na Maafisa Vijana kutoka Halmashauri zote nchini.