NILIACHA VYOTE KWA AJILI YA MERU MWIGULU : WANA, ARUMERU MMELAMBA DUME , MMEPEWA KIJANA SHUPAVU MWENYE WIVU WA MAENDELEO ..

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na Geofrey Stephen  Arumeru

Mgombea ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joshua Nasari, amezindua rasmi kampeni zake kwa hamasa kubwa katika Kata ya Ngarananyuki, akiahidi kuleta mapinduzi ya kimaendeleo yatakayobadili sura ya jimbo hilo.

Habari Picha 2945

Mkutano huo uliofurika maelfu ya wananchi ulipambwa na shamrashamra, huku ukihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha na Mgombea Ubunge wa Iramba, Mwigulu Nchemba, ambaye alimnadi Nasari kama “kijana shupavu, mzalendo na mpambanaji wa kweli.”

Kuacha Ukuu wa Wilaya kwa Ajili ya Wananchi.

Habari Picha 2946

Akihutubia kwa sauti ya msisitizo, Nasari alisema uamuzi wake wa kuacha nafasi ya ukuu wa wilaya aliyoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan haukuwa rahisi, lakini aliona ni lazima arudi nyumbani kuwatumikia wananchi wake.

“Nilikuwa nalindwa na askari wenye silaha, nina gari lenye kiyoyozi na nyumba nzuri. Lakini niliamua kuacha hayo yote ili nije kuomba kazi ya wananchi—kazi yenye changamoto nyingi—kwa sababu najua Meru imesahaulika kwa muda mrefu,” alisema huku akishangiliwa na umati.

Kipaumbele: Barabara na Maji Safi

Katika ahadi zake, Nasari alisema atapigania kwa nguvu zote upatikanaji wa barabara za lami na maji safi na salama, akitaja barabara ya Ngarananyuki–King’ori na ile ya Kikatiti–Sakila kama miradi ya kipaumbele

Habari Picha 2947

“Meru imezungukwa na milima, lakini cha ajabu wananchi wake hawana maji safi. Nikipewa ridhaa nitahakikisha changamoto hii inapata majibu ya haraka,” alisisitiza.

Sifa Kutoka kwa Viongozi na Wananchi

Waziri Mwigulu Nchemba alimnadi Nasari kwa nguvu, akieleza kuwa hata akiwa katika chama kingine zamani, alihangaika mara kwa mara kupigania maendeleo ya Meru.

“Sasa mmeshapata kijana jasiri na mzalendo. Nasari si mtu wa maneno matupu, bali ni mpambanaji wa kweli,” alisema.

Habari Picha 2955

Kwa upande wao, wananchi wa Ngarananyuki walionekana kumkubali mgombea huyo. Theresia Kaaya, mkazi wa eneo hilo, alisema:

Habari Picha 2948

“Kijana huyu amezaliwa hapa, anajua shida zetu na tunaamini atatuletea mabadiliko tuliyoyakosa kwa muda mrefu.”

Habari Picha 2954
Habari Picha 2953

Vilevile, mgombea udiwani wa CCM Kata ya Ngarananyuki, Happy Saanya, aliahidi wananchi wa kata hiyo kumpa Nasari kura za kishindo, akisema Ngarananyuki ni “lango la maendeleo ya Meru.”

 

Habari Picha 2949

Hali ya Kisiasa

Uzinduzi wa kampeni hizi umeibua matumaini mapya miongoni mwa wananchi wa Arumeru Mashariki, huku CCM ikijipanga kuhakikisha inashinda jimbo hilo ambalo limekuwa na historia ya kisiasa yenye ushindani mkali.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment