Wanahabari Watakiwa Kuandika Habari za Amani na Kuzingatia Usalama Wao
Mwandishi Wetu
Taasisi ya Waandishi wa Habari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) imetoa mafunzo kwa wanahabari kutoka mikoa mbalimbali nchini kuhusu namna ya kuandika habari zinazochochea amani pamoja na kulinda usalama wao wanapotekeleza majukumu yao, hasa wakati wa migogoro.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha wanahabari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Mara, Manyara, Mbeya na Arusha, na yalidhaminiwa na shirika la kimataifa la Press Unlimited.
Msisitizo wa Uandishi wa Amani.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, aliwataka wanahabari kuandika habari zinazohamasisha amani na mshikamano wa jamii badala ya kuchochea migogoro.
Alisema kuwa habari za upande mmoja zisizozingatia maadili ya taaluma na maslahi mapana ya umma zimekuwa zikichangia kuibuka au kuongezeka kwa migogoro katika jamii.


“Ni muhimu kujiuliza habari ina madhara gani na ina faida gani kwa jamii. Tusiwe na upendeleo katika uandishi wetu na tuzingatie tahadhari za kiusalama, hususan tunapotumia vyombo vya kidijitali pamoja na kulinda usalama binafsi,” alisema Juma.
Aidha, aliwahimiza wanahabari kufanya uchambuzi wa kina kabla na baada ya kuchapisha habari ili kuhakikisha taarifa wanazotoa hazileti madhara kwa jamii wala kwao wenyewe.
Kuzingatia Sheria za Habari.
Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea John Sendodo alitoa mada kuhusu sheria mbalimbali zinazosimamia sekta ya habari nchini. Aliwataka wanahabari kuzifahamu na kuzizingatia sheria hizo hata pale wanapoona zina mapungufu.
Baadhi ya sheria alizozitaja ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015, pamoja na Kanuni za Maudhui ya Mitandaoni.


Maadili ya Uandishi na Ubora wa Habari.
Mmiliki wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha Fanikiwa kilichopo Arusha, Joseph Mayagilla, alieleza umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo wakati wote wa utekelezaji wa majukumu ya uandishi.
Alisema kuwa kuongezeka kwa habari za upande mmoja na uandishi usiozingatia maadili kumeleta madhara katika jamii.
Mayagilla alipendekeza kurejeshwa kwa madawati maalum ndani ya vyombo vya habari, ikiwemo madawati ya habari za uchunguzi, amani na maendeleo, uchumi na mengineyo. Alieleza kuwa madawati hayo yakiongozwa na waandishi wabobezi yataongeza ubora na weledi wa habari.


Afya ya Akili kwa Wanahabari.
Mtaalamu wa saikolojia, Ester Cornelio, aliwataka wanahabari wanaokabiliwa na msongo wa mawazo kutafuta msaada wa kitaalamu badala ya kujifungia au kutumia njia zisizofaa kama vile unywaji wa pombe kupita kiasi au uvutaji wa sigara.
Alisema msongo wa mawazo (trauma) hauondolewi kwa matumizi ya vileo au sigara, bali kwa kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu.
Cornelio alibainisha kuwa wanaume wamekuwa wahanga zaidi wa msongo wa mawazo kwa sababu mara nyingi hushindwa kueleza hisia zao, tofauti na wanawake ambao huwa wazi zaidi kuzungumza.


Wito wa Mafunzo Endelevu.
Wakichangia mada, wanahabari Tausi Mbowe, Meneja wa Dawati la Kidijitali Star TV, na Anthony Mayunga kutoka Serengeti Media, walisisitiza umuhimu wa kuimarisha maadili ya uandishi pamoja na kuendelea kutoa mafunzo kuhusu sheria na afya ya akili kwa wanahabari.
Wanahabari wengine waliochangia ni Elizabeth Nyivambe (Mbeya), Muta Robert (Geita) na Zakaria Mtigandi (Manyara), ambao walieleza umuhimu wa kuendeleza mafunzo hususan katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na masuala ya usalama wa wanahabari.


Mwisho.



