Na OWM–TAMISEMI, Njombe
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha masoko ya kisasa nchini yanajengwa yakiwa na vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, ili kuwawezesha wanawake wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi bila vikwazo vya malezi ya watoto.

Hatua hiyo imebainishwa Februari 11, 2026 wakati wa ziara ya mafunzo kuhusu huduma za malezi na makuzi ya watoto yanayofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, yakihusisha watumishi kutoka OWM–TAMISEMI jijini Dodoma na Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Azimio la Kizazi cha Usawa wa Kiuchumi nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia afya Prof. Tumaini Nagu, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ustawi wa Jamii OWM–TAMISEMI, Bi. Subisya Kabuje, amesema Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha ustawi wa mtoto unaenda sambamba na uwezeshaji wa mwanamke kiuchumi.

Amesema maagizo ya Mhe. Rais yaliyotolewa Februari 8, 2026 wakati wa uzinduzi wa Soko Jipya la Kariakoo jijini Dar es Salaam yameweka mwelekeo mpya wa ujenzi wa masoko ya kisasa kwa kuzingatia huduma jumuishi, ikiwemo vituo vya kulelea watoto wadogo mchana.
Ameeleza kuwa kupitia vituo hivyo, kina mama wafanyabiashara wanapata uhakika wa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa utulivu, huku watoto wakipata huduma salama, malezi bora, lishe yenye ubora na mazingira rafiki kwa ukuaji wa afya na akili.
Ameongeza kuwa huduma hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya usalama wa mtoto kiafya na kisaikolojia pamoja na uwepo wa wahudumu waliopata mafunzo ya malezi na makuzi ya watoto wadogo.
Kwa upande wake, Bi. Alinine Msemwa amesema Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) inaendelea kuimarisha mazingira rafiki kwa watoto katika masoko yanayoendelea kujengwa nchini Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma za kulelea watoto mchana zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu, ili kumuwezesha mama mfanyabiashara kuongeza uzalishaji na kipato bila hofu juu ya usalama wa mtoto wake.


Mpango huo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Serikali wa kulinda na kuendeleza kizazi cha baadaye, sambamba na utekelezaji wa sera za maendeleo jumuishi zinazomuweka mwanamke na mtoto katikati ya ajenda ya maendeleo ya taifa.
Mwisho…



