MWEKEZAJI RANCHI SIHA ALIA BAADA YA MABOMA YA MIFUGO KUCHOMWA MOTO 🔥

Geofrey Stephen
3 Min Read

Siha, Kilimanjaro –

Mwekezaji anayefanya shughuli za ufugaji katika eneo la Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO), West Kilimanjaro wilayani Siha, ameomba Serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaodaiwa kuvamia na kuchoma mali zake, zikiwemo maboma ya mifugo.

Tukio hilo limeripotiwa kutokea mchana wa Februari 3, 2026, katika eneo la NARCO West Kilimanjaro, ambapo mwekezaji huyo alikuwa amekodisha kitalu kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Habari Picha 6679
Habari Picha 6678

Hasara Kubwa Yaripotiwa.

Akizungumza eneo la tukio, Bitres Laizer, mke wa mwekezaji John Kimiti, alisema tukio hilo limesababisha hasara kubwa na kuwaacha bila mahali salama pa kuhifadhi mifugo yao.

“Tunaomba Serikali ilisimamie jambo hili na itende haki. Mifugo yetu haina mahali pa kukaa, tumelazimika kulala porini kwenye baridi. Inasikitisha kuona mali zikiharibiwa wakati sisi tupo kisheria,” alisema kwa huzuni.

Bitres, mkazi wa Longido mkoani Arusha, alisema alipigiwa simu na wafanyakazi wake majira ya saa nane mchana.

wakimjulisha kuwa maboma ya mifugo yalikuwa yakiteketea kwa moto. Mbali na maboma, nyumba mbili ndogo za wafanyakazi, magodoro, vitanda, genereta, madumu ya maji na mali nyingine ziliteketea. Ndama mmoja aliripotiwa kuathirika, huku mifugo mingine ikiokoka kwa kuwa ilikuwa malishoni.

Habari Picha 6680
Habari Picha 6681

Taarifa Polisi na Kwa Mkuu wa Wilaya.

Baada ya tukio, taarifa zilitolewa Kituo cha Polisi Sanya Juu pamoja na kwa Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, ambaye alifika eneo la tukio kujionea uharibifu.

Bitres alieleza kuwa walikuwa wamepewa kitalu hicho na NARCO baada ya kuhamishwa kutoka eneo la awali, na walikuwa wamekaa hapo kwa takribani mwezi mmoja tu.

Alisema baadhi ya majirani hawakufurahishwa na uwepo wao.
Alidai aliwahi kuwaita viongozi wa kimila (Malegwanani) na majirani kwa lengo la kujitambulisha na kujenga ujirani mwema, lakini kikao kilichopangwa Januari 9, 2026 hakikufanyika.

Habari Picha 6682
Habari Picha 6683

Baadaye alipata taarifa za uwepo wa maandamano yaliyolenga kumwondoa kwenye eneo hilo, jambo alilolifikisha kwa vyombo vya dola na uongozi wa NARCO.

Mvutano waendelea Licha ya Jitihada za Usuluhishi.

Inadaiwa Januari 30, 2026 askari walifika eneo hilo kufuatia tahadhari ya kiusalama, na baadaye kamati ya usalama ya wilaya ilizungumza na wananchi waliodai hawamtaki mwekezaji huyo. Timu ya ufuatiliaji iliundwa ikiwahusisha viongozi wa kimila, huku mwekezaji akiombwa kusubiri majibu.

Hata hivyo, wakati akisubiri uamuzi,

wafugaji waliendelea kuingiza mifugo kwenye kitalu hicho. Bitres anadai watu kutoka vijiji vya Lekrumuni, Mawasiliano, Ndinyika na Magadini walivamia eneo lake lenye ekari 1,460 na kuchoma maboma pamoja na mali nyingine.

Habari Picha 6684

Wito wa Amani Watolewa.

Mkazi mmoja wa jamii hiyo, Mathias Nditika, alilaani tukio hilo akisema si utamaduni wa Wamasai kuchoma maboma, na kusisitiza kuwa maeneo ya Serikali yana taratibu za kufuatwa.

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment